1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Blinken aiomba China kuidhibiti Korea Kaskazini

9 Novemba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ameonya kwamba uhusiano wa kijeshi kati ya Korea Kaskazini na Urusi "unazidi kukua na ni hatari", na kuitaka China kuizuia Pyongyang.

https://p.dw.com/p/4YbUK
Japan Tokio US-Außenminister Blinken
Picha: Jonathan Ernst/Reuters/AP/picture alliance

Blinken ameyasema haya katika ziara yake huko Seoul kufuatia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 nchini Japan, na amekutana na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol pamoja na maafisa wengine wakuu leo Alhamisi.

Soma pia: Mkutano wa G7 walaani hatua za Korea Kaskazini kuipatia Urusi silaha

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini Park Jin amesema kwamba wamejadili pia kile kinachojulikana kama mkakati uliorefushwa wa uzuiaji kwa ajili ya kukabiliana na vitisho kutoka Korea Kaskazini, ikimaanisha matumizi ya vifaa vya kijeshi pamoja na zana na nyenzo za Marekani za kuweka ulinzi dhidi ya mashambulizi ya nyuklia, na kuboresha ushirikiano na Japan.

Marekani, Korea Kusini na Japan katika wiki za hivi karibuni zimeikosoa mara kwa mara Korea Kaskazini kwa kuisaidia Urusi kuendeleza vita vyake nchini Ukraine, huku Seoul ikisema kuwa Pyongyang inapata teknolojia ya anga kwa  kubadilishana na silaha na zana za kivita.

Hata hivyo Ikulu ya Kremlin mwezi uliopita ilisema "hakuna uthibitisho"  kwamba Korea Kaskazini imekuwa ikituma silaha kwa Urusi.

Akizungumza na waandishi wa habari Blinken amesema Marekani na Korea Kusini "zinashiriki wasiwasi mkubwa kuhusu ushirikiano wa kijeshi unaokua na wa hatari wa DPRK na Urusi", akitumia jina rasmi la Korea Kaskazini.

"Kuhusiana na msaada ambao Urusi inaweza kuwa inatoa kwa Korea Kaskazini. Hili ni jambo ambalo tunalitazama sana, kwa karibu sana, kwa uangalifu sana. Na bila shaka, tuna wasiwasi kuhusu msaada wowote kwa programu za makombora ya masafa marefu ya Korea Kaskazini, kwa teknolojia yake ya nyuklia na kwa uwezo wake.

"Na kama tulivyosema hapo awali, uungwaji mkono huo utakuwa ukiukaji wa wazi wa maazimio mengi ya usalama.Urusi ina wajibu, hasa kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, kushikilia maazimio hayo. sio kukiuka." Alisema Blinken.

soma pia: Lavrov aitembelea Korea Kaskazini

Uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Urusi

Nordkorea | Militärparade in Pjöngjang
Zana za vita za Korea KaskaziniPicha: KCNA/KNS/AP/picture alliance

Urusi na Korea Kaskazini ni washirika wa kihistoria ambao wote wako chini ya vikwazo vya kimataifa, Urusi kwa uvamizi wake Ukraine na Korea Kaskazini juu ya silaha zake za nyuklia na programu za makombora.

Katika mikutano ya awali, Blinken na mshauri wa usalama wa taifa wa Korea Kusini Cho Tae-yong waliilaani Korea Kaskazini kwa kutuma silaha kwa Urusi kwa matumizi nchini Ukraine.

 Korea Kusini ni msafirishaji mkuu wa silaha, lakini sera ya muda mrefu inaizuia kutuma silaha katika maeneo yenye migogoro. Hata hivyo wachambuzi wanahoji kwamba Korea Kusini itaendelea kukabiliwa na shinikizo la Marekani ili kuendelea kufuata msimamo huo.

 

//Reuters, AFP