1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken na Lavrov wajadili kurejesha mahusiano.

Sudi Mnette
20 Mei 2021

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi wakutana kwa mara ya kwanza na kudali tofauti zilizopo baina ya mataifa hayo mawili kwa lengo la kuzitafutia ufumbuizi.

https://p.dw.com/p/3tdy9
Island Antony Blinken und Sergey Lavrov in Reykjavík
Picha: Saul Loeb/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken na mwenziwe wa Urusi, Sergei Lavrov wamejadili kurejesha mahusiano wa mataifa yao katika hali njema, baada ya kukutana katika mkutano wa ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu Rais Joe Biden aingie madarakani huko nchini Iceland.

Mawaziri  hao wa mambo ya nje wameonekana wakiwa katika jitihada ya kupunguza hali ya mvutano baina ya mataifa yao mawili ambapo wote kwa pamoja wakisema wapo tayari kushirikiana huku wakikiri uwepo wa tofauti kubwa inayowatenganisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Blinken amesema Marekani inataka mahusiano yenye kuonesha dira, madhubiti na Urusi, katika kikao chake hicho na Lavrov kilichofanyika kabla ya mkutano wa kilele wa mawaziri wa mataifa yaliyo katika baraza la mataifa ya Aktiki.

Marekani na Urusi zina tofauti kubwa.

Russland Krim | Abzug des Militärs nach Manöver
Jeshi la Urusi katika eneo la CrimeaPicha: Russian Defense Ministry/AP/picture alliance

Lakini aliongeza kusema si siri kwamba Marekani na Urusi zinatofauti kwa sasa, na kwa kuzizingatia Rais Joe Biden amemweka wazi kabisa mwenziwe wa Urusi, Vladimir Putin, atambue kama Urusi ikichukua hatua kali dhidi ya Marekani au hata washirika wao na Marekani itajibu mapigo kwa kufanya hivyo. Lakini pia aliongeza kusema "Na kama Rais Biden alivyozungumza na Rais Putin, tunatafuta uhusiano wenye kutabirika, uliothabiti na Urusi. Tunadhani hatua hiyo ni njema kwa watu wetu, nzuri kwa watu wa pia Urusi, na, hakika, nzuri kwa ulimwengu wote."

Urusi inataka mjadala wa heshima na kuaminiana na Marekani

Nae Lavrov alijibu kwa kusema mataifa hayo mawali yanatofauti kubwa pale inapohusika tathimini ya hali ya kimataifa na kwambo wapo katika muelekeo wa jitihada za kulitatua jambo hilo. Aidha waziri huyo wa mambo ya nje wa Urusi aliongeza kwa kusema taifa lake lipo tayari kuyaweka maswala yote mezani kwa zingatio la kwamba mjadala wake utakuwa wenye kubeba ukweli na kuaminiana. Zaidi aliongeza "Ni dhahiri, muhimu sana kwa uhusiano wetu, kwetu sisi kuamua namna gani tutakavyojenga uhusiano zaidi, kama marais wetu wanavyotaka."

Wanadplomasia hao wa juu wanatarajiwa pia kujadili kuhusu uwezekano wa kufanyika mkutano kati ya Rais Biden na Rais wa Urusi Vladmir Putin. Rais Biden alitoa pendekezo la kufanyika mkutano nje ya mataifa yao, wazo ambalo hadi sasa halijawa wazi kama litakubaliwa na Rais Putin.

Mada nyingine ambazo zilipata nafasi katika mazungumzo haya ya sasa kati ya Lavrov na Blinken ni pamoja na mgogoro wa Israel na Palestina, Mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini na Iran pamoja na hali ilivyo tete huko Afghanistan.

Chanzo: DPA