1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram yakiri kuwateka nyara mamia ya wanafunzi

15 Desemba 2020

Kundi la Boko Haram limedai kuhusika na utekaji nyara wa mamia ya wanafunzi kaskazini magharibi mwa Nigeria, katika kile kinachoonekana kuwa ni upanuzi mkubwa wa shughuli za kundi hilo katika maeneo mapya

https://p.dw.com/p/3mjz5
Nigeria Kankara | Angriff auf Schule | Entführte Schulkinder
Picha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Kiasi ya wanafunzi 333 bado hawajulikani walipo tangu shambulizi la Ijumaa usiku kwenye shule moja ya wavulana ya sekondari katika jimbo la Katsina - iliyoko mamia ya kilomita kutoka ngome ya Boko Haram ya kaskazini mashariki mwa Nigeria. Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, ameyasema hayo kwenye mkanda wa sauti ijapokuwa ni vigumu kuithibitisha sauti hiyo.

Zaidi ya watu 100 waliobeba bunduki na kutumia pikipiki walivamia shule hiyo katika mji wa Kankara, na kuwalazimu wanafunzi kukimbia na kujificha kichakani. Jeshi limesema limeyagundua maficho yao na kuwa operesheni ya kijeshi inaendelea.

“Kilichofanyika Katsina kimefanywa ili kuhimiza Uislamu na kuondoa shughuli zilizo kinyume na Uislam wakati elimu ya magharibi sio elimu iliyoamriwa na Allah na Mtume”, gazeti hilo limemnukuu Shekau.

Msemaji wa rai swa Nigeria Garba Shehu, alisema katika kauli yake jana Jumatatu kwamba ”watekaji wamefanya mawasiliano na mazungumzo ya kuwarejesha na usalama” wa wanafunzi hao nyumbani kwao.

Makundi kadhaa yaliyo na silaha yanaendesha shughuli zake kaskazini Magharibi mwa Nigeria uliko mji wa Katsina. Hapo awali iliaminika kuwa watekaji huenda ni wahalifu ambao mara nyingine hufanya kazi na Boko Haram.

Boko Haram imewahi kuwateka wanafunzi katika kipindi cha nyuma. Utekaji mkubwa ulikuwa ni ule wa mwaka 2014 ambapo wanafunzi wa kike zaidi ya 270 walitekwa katika mabweni yao huko Chibok.