1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolsonaro atumia kongamano la Davos kuvutia wawekezaji

Sylvia Mwehozi
23 Januari 2019

Rais mpya wa Brazil Jair Bolsonaro amelitumia jukwaa la kongamano la kiuchumi linalofanyika mjini Davos Uswisi, kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wa kigeni akisema serikali yake itaimarika kiuwekezaji.

https://p.dw.com/p/3C0HQ
Weltwirtschaftsforum 2019 in Davos | Jair Bolsonaro, Präsident Brasilien
Picha: picture-alliance/dpa/Keystone/G. Ehrenzeller

Bolsonaro ameahidi kufungua uchumi wa Brazil, kupunguza na kurahisisha kodi, kuyabinafsisha makampuni ya taifa na kumpatia waziri wake wa sheria nguvu ya kupambana na ufisadi. Ameapa kurejesha utulivu wa kiuchumi na nidhamu ya kifedha, ingawa hakugusia mageuzi ya pensheni kama moja ya changamoto kubwa katika kudhibiti nakisi katika bajeti. Uhifadhi wa mazingira na viumbe hai ni miongoni mwa mikakati ya rais huyo mpya aliye na siasa za mrengo wa kulia.

"Mazingira lazima yaendana na maendeleo. Hakuna kuegemea upande mmoja. Kilimo cha biashara ni chini ya asilimia 9 ya eneo letu nchi nzima huku mifugo ikichukua asilimia 20. Leo hii asilimia 30 ya ardhi ya Brazil ni misitu, sisi ni mfano wa kuigwa na dunia. Tutafanya maboresho inapowezekana ili kupunguza gesi ya kaboni na kuhifadhi mazingira, "alisema Bolsonaro.

Siasa za Ulaya na Asia zitagubika kongamano hilo siku ya Jumatano, wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe watakapowahutubia wajumbe wa kongamano. Merkel anatarajiwa kugusia juu ya Umoja wa Ulaya na masuala kadhaa ya kimataifa, wakati taifa hilo likishikilia kiti kisicho cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Interview Tony Blair DW Weltwirtschaftsforum Davos
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair akizungumza na DW, mjini DavosPicha: DW/J. Gottschalk

Wengine watakaohutubia ni pamoja na Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte, waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, sambamba na wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka Canada, China na Korea Kusini. Mbali ya vita vya kibiashara, wajumbe katika kongamano la Davos wana wasiwasi na kushuka kwa ukuaji uchumi wa China.

Mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya-Brexit pia utajitokeza katika mazungumzo ya Davos, ambapo waziri wa biashara wa Uingereza Liam Fox ameahidi kukutana na mawaziri wa biashara ili kujadiliana mustakabali wa nchi yake baada ya kujiondoa kwenye makubaliano ya biashara ya Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair amesisitiza haja ya kufanyika kura ya pili ya maoni kuhusiana na taifa hilo kujiondoa Umoja wa Ulaya. Akizungumza na DW pembezoni mwa kongamano la Davos, Blair amesema kutokana na mgogoro uliopo bungeni, jambo la busara ni kurejea kwa watu ili wafanye maamuzi. Amekosoa mipango yote ya Brexit ambayo inajadiliwa hivi sasa, na kuongeza kwamba ikiwa Uingereza itasalia kwenye umoja wa forodha au soko la pamoja la Umoja wa Ulaya, itakuwa na wajibu wa kufuata kanuni za Umoja huo na bila kuwa na kauli katika maamuzi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters/dpa/Afp

Mhariri: Daniel Gakuba