1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson akutana na Leo Varadkar kuhusu Brexit

Oumilkheir Hamidou
9 Septemba 2019

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekuwa na ya mazungumzo pamoja na kiongozi mwenzake wa jamhuri ya Ireland Leo Varadkar wakati ambapo mpango wa kuitoa Uingereza katika umoja wa Ulaya Brexit unadhihirka kukwama.

https://p.dw.com/p/3PIXg
Irland Dublin Leo Varadkar empfängt Boris Johnson
Picha: Getty Images/AFP/C. McQuillan

Waziri mkuu wa Uingereza  Boris Johnson amekutana na kiongozi mwenzake wa jamhuri ya Ireland  Leo Varadkar katika juhudi za  kuuokoa mkakati wake wa kuitoa kwa kila hali nchi yake kutoka Umoja wa Ulaya ,Brexit na kulazimisha uchaguzi wa mapema licha ya upinzani mkali katika bunge la nchi hiyo. 

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikuwa na mazungumzo pamoja na kiongozi mwenzake wa jamhuri ya Ireland Leo Varadkar mnamo wakati ambapo utaratibu wa kuitoa Uingereza katika umoja wa Ulaya Brexit unadhihirka umekwama na wabunge wa nchi hiyo ya kifalme wakionyesha wamepania kulipinga kwa mara nyengine tena pendekezo lake la kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati mwezi unaokuja.

Hakuna maridhiano yaliyofikiwa pia wakati wa mazungumzo yao. Katika taarifa yao ya pamoja viongozi hao wawili wamesema tu "mkutano wa mjini Dublin ulikuwa wa maana."Boris Johnson amehaakikisha anataka Uingereza itoke katika umoja wa ulaya kwa maridhiano.Taarifa hiyo ya pamoja imesema tu viongozi hao wawili wanapanga kukutana tena hivi karibuni. Suala la mpaka kati ya jamhuri ya Irelad na jimbo la Ireland linaangaliwa kuwa mzizi wa fitina uliosababisha kukwama utaratibu wa Brexit.

Mchakato wa Brexit ulisababisha mtangulizi wa Boris Johnson, bi Theresa May kujiuzulu, na hata kwa Johnson, mchakato huo haujampa utulivu wowote kisiasa tangu achukue usukani.
Mchakato wa Brexit ulisababisha mtangulizi wa Boris Johnson, bi Theresa May kujiuzulu, na hata kwa Johnson, mchakato huo haujampa utulivu wowote kisiasa tangu achukue usukani.Picha: Reuters/PA Wire/D. Lawson

Serikali ya waziri mkuu Boris Johnson imethibitisha bunge litafungwa hadi October 14 inayokuja, baada ya kikao cha leo usiku bila ya kujali matokeo ya kura  kuhusu pendekezo la waziri mkuu la kuitisha uchaguzi mkuu wa kabla ya wakati. Wabunge walio wengi wameshasema watalipinga kwa mara nyengine tena pendekezo hilo. Upande wa upinzani unahofia Boris Johnson  asije akadharau sheria waliyoipigia kura wiki iliyopita kwa msaada wa wahafidhina walio asi, sheria inayomlazimisha waziri mkuu auombe Umoja wa ulaya urefushe kwa miezi mitatu mchakato wa Brexit.

Wakati huo huo mshauri wa zamani wa serikali ameashiria Boris Johnson atapoteza idadi ya viti akilinganishwa na mtangulizi wake Theresa May pindi uchaguzi mkuu ukiitishwa. Waziri mkuu wa zamani alijipatia viti 318 kati ya 650 vya bunge mnamo mwaka 2017 , mataokeo yaliyomlazimisha kuungana na chama kidogo cha Ireland ya kaskazini ili kuweza kuunda serikali. Boris Johnson amepoteza wingi wa viti bungeni baada ya baadhi ya wabunge wa kihafidhina kumpa kisogo na wengine 21 kufukuzwa chamani kwasababu ya msimamo wao dhidi ya utaratibu wa kujitoa katika umoja wa ulaya bila ya maridhiano.

Vyanzo: Reuters/dpa