1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi ziarani Syria

30 Oktoba 2013

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Lakhdar Brahimi, anakwenda Syria huku juhudi za kimataifa za kuzikutanisha pande zinazohusika na mzozo wa Syria zikikabiliwa na upinzani wa makundi ya itikadi kali.

https://p.dw.com/p/1A78L
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa kwa Syria Lakahdar BrahimiPicha: Reuters

Brahimi yuko ziarani mjini Damascus kujaribu kuzitanabahisha pande zinazohusika na mzozo wa Syria zishiriki katika mazungumzo ya amani ya Geneva katika wakati ambapo makundi ya waasi yanayataja mazungumzo hayo kuwa ni ya uhaini.

Ziara hiyo inafanyika katika wakati ambapo makundi zaidi ya 20 ya wanamgambo yametangaza upinzani wao dhidi ya mkutano wa kimataifa wa amani ya Syria, ikiwa hautapelekea kung'olewa madarakani Rais Bashar al-Assad.

"Ufumbuzi wowote ambao hautahitimisha enzi za utawala wa Assad na kubebeshwa jukumu wale wote waliochangia katika visa vya uhalifu,utapingwa moja kwa moja," wameonya wanamgambo hao katika taarifa yao inayodai kushiriki katika duru ya pili ya mazungumzo ya Geneva kwa masharti tofauti na hayo waliyoyataja "ni sawa na uhaini."

Wanamgambo hao wanatishia kumhukumu kwa makosa ya uhaini mwanaharakati yeyote wa upinzani atakaeshiriki katika mazungumzo hayo ya Geneva.

Taarifa hiyo imetiwa saini na makundi 22 ya wanamgambo,mengi kati yao yakiwa ya itikadi kali,yakiwemo Souqour al-Charm, al Tawhid na Ahfad al-Rassoul yanayosemekana yanaungwa mkono na Qatar pamoja pia na wanamgambo wa Ahrar al-Char , mojawapo ya makundi mashuhuri yanayopigana mashariki ya Syria na Al Sahaba wanaoendesha opereshini zao katika eneo la mji mkuu Damascus.

Urusi yawakaripia wapinzani

Krieg in Syrien ARCHIVBILD 04.04.2013
Wanamgambo wa itikadi kaliPicha: Guillaume Briquet/AFP/Getty Images

Urusi, mwandalizi mwenza pamoja na Marekani wa mazungumzo hayo imeukosoa vikali msimamo wa waasi.

"Ujeuri mkubwa huu kuwaona wafuasi wa itikadi kali, mashirika ya kigaidi yanayopigana dhidi ya vikosi vya serikali wakiwatisha wale wenye moyo wa kutaka kushiriki katika mazungumzo," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Ratiba halisi ya duru ya pili ya mkutano wa kimataifa wa amani ya Syria mjini Geneva haijatangazwa rasmi, lakini viongozi kadhaa akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil El-Arabi, wanasema huenda yatafanyika baadaye mwezi ujao.

Makundi ya upinzani ya Syria, ambayo tokea hapo hayana msimamo mmoja linapohusika suala la mazungumzo ya amani, yanapanga kukutana tarehe 9 Novemba nchini Uturuki.

Hata hivyo, msimamo huu mkali wa makundi ya wanamgambo unakorofisha juhudi za Brahimi mjini Damascus.

Syria yakabidhi orodha ya silaha za kemikali

Wakati huo huo shirika linalosimamia kupigwa marufuku silaha za kemikali limesema Syria imewakabidhi ratiba ya kuteketeza silaha zake za kemikali, hiyo ikiwa awamu nyengine ya Azimio Nambari 2118 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka silaha za kemikali za Syria ziteketezwe hadi ifikapo katikati ya mwaka 2014.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu