1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Mawaziri wa May wapanga kumuondoa madarakani

Iddi Ssessanga
24 Machi 2019

Vyombo vya habari nchini Uingereza vinaripoti kuwa baraza la Theresa May linakataa kuunga mkono uongozi wake na linamtaka aachie madaraka. Kiongozi wa muda atateuliwa kusimamia majadiliano ya Brexit

https://p.dw.com/p/3FZtC
Belgien Brüssel EU Treffen | Theresa May
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti Jumamosi usiku kwamba waziri mkuu Theresa May alikuwa anakabiliwa na uasi ndani ya baraza lake la mawaziri na huenda akajiuzulu mara moja. Hatua hiyo inakuja siku chache kabla ya kura ya tatu kuhusu makubaliano ya May juu ya Brexit yaliokatiliwa mara mbili.

Tunachokijua mpaka sasa:

  • Magazeti ya The Sunday Times, The Telegraph na The Daily Mail yaliripoti juu ya uwezekano wa mapinduzi, yakiwanukuu wabunge wa chama cha Conservative.
  • Yote yalisema kiongozi wa muda atachaguliwa kusimamia wiki za mwisho za mchakato wa Brexit.
  • Gazeti la udaku la The Daily Mail lilisema waziri wa Mazingira Michael Gove huenda akachukuwa uongozi wa mpito kabla ya kinyang'anyiro kamili msimu wa joto.
  • THe Sunday Times 24.03.2019 Titel
    Gazeti la The Sunday Times likiongoza na habari ya mapinduzi ya baraza la mawaziri dhidi ya May.Picha: The Sunday Times

'Dhihaka'

Mhariri wa siasa wa gazeti la The Times Tim Shipman alisema "mawaziri wamemgeuka May kwa namna ya kushangaza," na wanamshinikiza kuondoka, ingawa bado hajachukuwa uamuzi thabiti kufanya hivyo. Aliongeza kuwa mume wa May alikuwa mojawapo ya wachache wanaomhimiza aendelee kuwepo kama waziri mkuu.

Mbunge anaeunga mkono Brexit Anne-Marie Trevelyan aliliambia gazetila The Telegraph kwamba namna May "alivyoruhusu kutendewa mjini Brussels ilifanyia dhihaka azma ya kurejesha udhibiti."

Mtandao wa Buzzfeed News ulisema mnadhimu wa serikali Paul Maynard alimuambia May kuwa mkakati wake ulikuwa unafeli na kukiharibu chama chao. Mbunge wa Conservative George Freeman aliielezea kwa muhtasari hali ya kisiasa, akisema "unaweza kuona hasira."

Maandamano makubwa London

Mapema siku ya Jumamosi, zaidi ya watu milioni moja waliandamana katika mitaa ya jiji la London kudai kura ya pili ya maoni, na kuhimitisha miaka miwili ya mashaka ya kisiasa. Mabango yalikuwa na ujumbe kwa serikali "kuondoa kifungu cha 50" na "tunaandamana kutaka kura ya watu" na pia "Tunaupenda Umoja wa Ulaya."

Maandamano hayo yalihdhuriwa na watu kutoka vyama vyote ambapo naibu kiongozi wa chama cha Labour Tom Watson alisema anaunga mkono kura ya pili ya maoni "kama njia pekee" ya kutatua mkwamo wa Brexit. Pia waziri kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon na kiongozi wa chama cha Liberal Democrats Vince Cable walishirkia maandamano hayo.

Großbritannien London People's Vote Demonstration
Waandamanaji wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kutaka kura nyingine ya Brexit.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Wigglesworth

Lakini si kiongozi wa Labour Jeremy Corbyn wala kansela kivuli John McDonnell waliokuwepo kwenye maandamano hayo. Meya wa London Sadiq Khan kutoka chama cha upinzani cha Labour alisema alikuwa anaandamana "pamoja na watu kutoka kila kona ya nchi, kutaka watu wa Uingereya wawe na kauli ya mwisho."

Mbunge wa chama cha Kijani Caroline Lucas alilinganisha mwitikio na maandamano ya dazeni chache za wafuasi waliotembea kutokea kaskazini mwa England kumuunga mkono mwasisi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha UK Independent UKIP, Nigel Farage.

Kura ya pili ya maoni

Ombi la matandaoni kwenye tovuti ya bunge likitoa wito wa kifungu cha 50 kusitishwa lilikuwa sahihi milioni 4.4 kufikia Jumamosi, licha ya tovuti hiyo kukwama mara kadhaa.

Mbunge wa zamani wa Conservative Anna Soubry aliacha chama chake mwezi Februari kujiunga na kundi huru na alisema alipokea vitisho vya kuuawa kuhusiana na msimamo wake kuhusu Brexit. Yeye pia alishiriki maandamano ya Jumamosi. "Tunaandamana kwa ajili ya nchi yetu - kwa ajili ya mustakabali wa watoto wetu na wajukuu zetu," aliandika kweye ukurasa wake wa Twitter.

Mbunge wa Conservative na mwanasheria mkuu wa zamani Dominic Grieve alimkosoa waziri mkuu May wiki iliyopita kwa kulilaumu bunge la wawakilishi kutokana na mgogoro wa Brexit, huku akikataa kukubali kubeba dhamana yoyote mwenyewe. Mwanasiasa huyo anaeunga mkono Umoja wa Ulaya aliwaambia wabunge kuwa: "Sijawahi kujisikia aibu kuwa mwanachama wa chama cha Conservative au kuombwa kumuunga mkono."

Großbritannien London People's Vote Demonstration
Naomba kurejeshewa mustakabali wangu, tafadhali, linasomeka bango hilo ambalo liliandikwa kifasihi na kujumlisha herufi za jina la waziri mkuu May.Picha: Imago/i Images/P. Maclaine

Hakuna kura ya tatu bungeni?

Waziri mkuu May amesema huenda asirejeshe tena makubaliano yake bungeni wiki ijayo ikiwa hakutakuwepo na uungwaji mkono wa kutosha kuweza kuyapitisha katika juhudi ya tatu. May aliwaandikia wabunge wote siku ya Ijumaa akipendekeza kuzungumza nao katika siku zijazo "wakati bunge likijianda kuchukuwa maamuzi ya maana sana."

Alisema kulikuwa na machaguo manne mbele ya wabunge hao:

  • Kupigia kura mpango wake kwa mara ya tatu - suala linalotegemea idhini ya spika wa bunge la wawakilishi John Bercow ambaye alisema kunapaswa kuwa na mabadiliko makubwa katika maandishi yaliopita ili kuupigia tena kura, akinukuu sheria ya mwaka 1604;
  • Kuwasilisha mpango mbadala kwa Umoja wa Ulaya kabla ya tarehe mpya ya mwisho ya Brexit Aprili 12;
  • Kusimamisha kifungu cha 50, ambacho kitakomesha machakato wa sasa wa Brexit inagawa hakizuwii mwingine, ambao May alisema "utasaliti matokeo ya kura ya maoni,"
  • Kuondoka Umoja wa Ulay abila makubaliano, suala ambalo bunge la wawakilisji lilipiga kura kulikataa wiki iliyopita.

May amesema kura nyingine ya wananchi itasababisha "janga la maumivu". Matokeo ya kura ya mwaka 2016 yalikuwa asilimia 52 upande wa kujitoa dhidi ya 48 waliounga mkono kubakia. Muda mpya wa kufikia makubaliano ni Aprili 12, ili kuepusha Uingereza kusimamisha wagombea katika uchaguzi ujao wa bunge la Ulaya mwezi Mei.