1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit, Ufaransa baada ya uchaguzi na SPD Magazetini

Oumilkheir Hamidou
20 Juni 2017

Mazungumzo ya kuachana Uingereza na Umoja wa Ulaya-Brexit, Ufaransa baada ya uchaguzi wa bunge na pendekezo la kodi ya mapato la chama cha SPD ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/2f0XS
Brüssel Beginn Brexit Verhandlungen Barnier und  Davis
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Tunaanzia Brussels yalikoanza mazungumzo yatakayopelekea kujitenga moja kwa moja Uingereza na Umoja wa Ulaya. Wahariri wanakubaliana talaka zinaanza kuandikwa. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika:"Utaratibu umeshaanza na mwisho wake si mwengine isipokuwa talaka. Wema na upole vitatoweka mara moja mada zitakapoanza kujadiliwa kwa kina. Kwasababu ingawa masahibu wa hadi wakati huu wanataka kuendelea kusikilizana, lakini hadi talaka zitakapotolewa watalazimika kuhasimiana. Wawakilishi wa Muungano wa kifalme wametambua zamani, wanajikuta katika njia ya hatari. Kulipa kisogo soko la pamoja, kujitenga na umoja wa forodha, na dalili za mfarakano kati ya Ulaya na Marekani, yote hayo yanaitenga zaidi London kuliko vile ilivyokuwa ikifikiriwa.

Yaliyopita yamepita

Gazeti la "Allgemeine Zeitung" la mjini Mainz linahisi, hata kama mazungumzo yameanza vizuri, haimaanishi kitu, mwisho wake  kwa kila hali ni wa uharibifu. Hata kama watu wanaunga mkono fikra ya kuitishwa kura ya maoni, lakini iwepo njia ya tatu, mfano kiunzi cha thuluthi  mbili, linapohusika suala la masilahi ya juu ya taifa. Hiyo ingezuwia kampeni za uchaguzi za wapinzani wa Umoja wa ulaya kueneza uwongo kuhusu Umoja wa ulaya. Pigo alilolipata waziri mkuu Theresa May katika uchaguzi wa bunge ni ushahidi  kamili wa kura ya dhidi ya Brexit. Lakini yamepita sasa. Kitakachofuata ni machungu."

Macron hana njia isipokuwa kuitumia fursa iliyoko

Uchaguzi wa bunge nchini Ufaransa nao pia umegonga vichwa vya habari nchini Ujerumani. Chama cha rais Emmanuel Macron kimejikingia wingi mkubwa wa viti kuweza kuanzisha mageuzi yaliyokusudiwa. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika:" Ufaransa  inahitaji mageuzi ikizingatiwa utaratibu wake wa watu kufanya kazi masaa 35 kwa wiki, watu  kuruhusiwa kustaafu mapema na zidi ya asili mia 9 ya wasiokuwa na kazi. Sera za kiuchumi zinakamata mstari wa mbele katika ajenda ya Macron. Fedha zinabidi ziwepo kabla ya kugawanywa. Baadhi ya wanaopigania masilahi ya wafanyakazi wameshatangaza watayapinga moja kwa moja mageuzi hayo, lakini wengine wameshaonyesha utayarifu wa kuyaunga mkono. Emmanuel Macron anabidi aitumie hali ya mwamko iliyochomoza ili kuanzisha haraka mipango ya mageuzi kabla ya gurudumu kugeuza njia. Rais mpya wa Ufaransa anapanga kusamehe mwaka huu likizo yake ili kuushughulikia mkakati wake. Anatambua hana wakati wa kupoteza.

SPD n pendekezo la kodi ya mapato

Mada yezu ya mwisho magazetini inahusiana na pendekezo la chama cha Social Democratic, SPD kuhusiana na kodi ya mapato. Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linahisi pendekezo hilo ni la busara na sawia. Wenye nguvu wabebeshwe mzigo mzito zaidi kuliko wenzao ambao mabega yao ni dhaifu. Kwa wenye kipato kidogo na cha wastani pendekezo hilo linamaanisha, kupunguziwa mzigo wa kodi na wenye mishahara mikubwa mikubwa watabidi wawajibike mbele ya idara za kodi za mapato. Kwa hivyo kila kitu ni sawa. Na muhimu zaidi ni kwamba SPD wanawanyooshea mkono hata wale ambao mapato yao ni madogo kwa namna ambayo hata kodi hawastahiki kulipa.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu