1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brown ahutubia mkutano mkuu wa chama chake cha Leba

Mohammed Abdul-Rahman24 Septemba 2007

Azungumzia mipango ya serikali yake kuimarisha huduma za jamii,ikiwemo elimu na afya na pia mpango wa hatua kali kupambana na wanaodhibiti silaha kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/CH7p
Waziri mkuu wa Uingereza na kiongozi wa chama cha Leba Gordon Brown
Waziri mkuu wa Uingereza na kiongozi wa chama cha Leba Gordon BrownPicha: AP

Waziri mkuu Gordon Brown alikaribishwa kwa heshima shangwe na hoi hoi na wajumbe mjini Bournemouth waliosimama kwa dakika kadhaa wakimpigia makofi hata kabla hajaanza hotuba yake. Katika hotuba yake aliwapongeza wajumbe akisema ni heshima kwake kuhutubia kwa mara ya kwanza akiwa kiongozi wa chama cha Leba, miezi mitatu baada ya kuchukua wadhifa wa Waziri mkuu kutoka kwa mtangulizi wake Tony Blair.

Alizungumzia juu ya matukio yaliopita ya hujuma za kigaidi mjini London na Scotland alivipongeza vyombo vya dola na raia wema waliotoa mchango katika kuhakikisha raia wanaoshi kwa usalama na bila hofu. Akazungumzia pia mchango na mshikamano katika kupambana na mafuriko ya mnamo msimu wa joto mwaka huu. Aidha alikumbusha kwamba ili kupata mafanikio ya kiuchumi , katika hifadhi ya mazingira na vita dhidi ya ugaidi, Uingereza itafanikiwa kwa kuwa taifa moja na sio Scotland, Wales, England au Ireland Kaskazini.

Akisisitiza juu ya azma na haja ya serikali yake kuimarisha kwa elimu Waziri mku Brown alielezea shukurani zake kwa nafasi ya elimu aliyopata , lakini akaelezea masikitiko yake kuwaona baadhi ya marafiki wa utotoni ambao hawakujaaliwa kupata nafasi hiyo, na hivyo kusisitiza kwamba lengo kubwa ni kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya elimu inavyopaswa. Na kwa yoyote anayetaka kupata elimu fedha kisiwe kikwazo. Akataja juu ya kusimama kidete kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya afya pamoja na kujenga Uingereza itakayowasimamia raia wake na nafasi za maisha kwa kila familia.

Lengo la chama cha Leba alisema Bw Brown ni kuwa chama cha maendeleo na mabadiliko, na Uingereaza haiwezi kupoteza ujuzi wa mtu yeyote. Nchi yenye kuleta manufaa kwa watu wake , hugeuka kuwa mafanikio pia kwa wengine duniani, alisema.

Suala lisiwe wewe ni anani , unamjua nani na umetoka wapi, bali ni ujuzi na maarifa yako yatakayokua ufunguo wa mafanikio yako binafsi . akazungumzia mpango wa miaka 10 kuimarisha elimu kwa jumla hadi chuo kikuu.Waziri mkuu huyo alizungumzia pia mafanikio ya kiuchumi na kusema leo hii jumla ya watu 29 milioni wana kazi nchini Uingereza.

Suala jengine lilikua la usalama na juhudi za kupambana na wimbi la uhalifu unaotokana na matumizi ya silaha. Akafafanua juu ya mipango ya vyomnbo vya dola kuimarisha juhudi za kuzuwia uingiaji wa bunduki kinyume cha sheria. Akapendekeza hatua kali ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka mitano kwa yeyote atakayemiliki silaha kinyume cha sheria.

Jengine ni hatua kali dhidi ya wanaohusika na biashara ya madawa ya kulevya .

Aidha kutakua na hatu kali za kudhitbii kuingia wahamiaji nchini kiholela na wageni watapewa vitambulisho ukaazi, lakini yeyote atakayegunduliwa anahusika na silaha au madawa ya kulevya ataondoshwa mara moja.

Katika kile kinachoangaliwa ni mabadiliko makubwa, Bw Brown alisema chama chake kina mpango wa kuleta mageuzi katika baraza la mabwanyenye-House of Lords-, kuhaklikisha wajumbe wanachaguliwa na sio kuteuliwa.

Masuala mengine ni ulinzi wa mazingira . alisema Uingereza itakua ya kwanza kupunguza utoaji wa hewa chafu inayochafua mazingira na kugeuza haja hiyo kuwa ya kisheria.

Katika uwanja wa kimataifa aliitaka serikali ya Sudan kupiga hatua ya maendeleo ili wanawake na watoto wa Darfur waishi kwa amani na usalama la si hivyo, au iwe tayari kukabiliwa na hatua kali ya vikwazo. Alimpongeza mtangulizi wake Tony blair akisema miongoni mwa mafanikio ni kuwa leo jamii mbili huko Ireland ya kaskazini zimegawana madaraka.

Kuhusu Irak na Afghanistan alisema watafanya kila wawezalo kwa ajili ya amani katika nchi hizo, pamoja na kushirikiana na washirika wote kupambana na kuzishinda hisia za imani na siasa kali.

Aidha Bw Brown alitaja pia haki ya kila mtu duniani kote kupata elimu , na matibabu ikiwa ni pamoja na kupambana na ukimwi. Kwa jumla hotuba ya Bw Brown iligusia masuala kuanzia ya kijamii na uchumi ya kimataifa.