1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brussels, London wasifu mfumo mpya kuhusu Ireland Kaskazini

Daniel Gakuba
28 Februari 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wa Uingereza wamesifu makubaliano waliyoyasaini Jumatatu kuhusu utaratibu wa biashara kati ya Ireland na Ireland Kaskazini, baada ya mwaka mzima wa malumbano na kuhasimiana kisiasa.

https://p.dw.com/p/4O4Ca
England Brexit Rishi Sunak und Ursula von der Leyen
Kutoka kushoto, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, na Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi SunakPicha: Steve Reigate/empics/picture alliance

Makubaliano hayo yaliyopachikwa jina la ''Windsor Framework'' yaliafikiwa kati ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen jana mjini London, yanaondoa vizuizi na ukaguzi wa bidhaa zinazotoka sehemu nyingine za Uingereza vikiingia Ireland Kaskazini, na kuwapa wabunge wa Ireland Kaskazini kauli yenye uzito mkubwa juu ya sheria za baadaye za Umoja wa Ulaya.

Soma zaidi: Uingereza na EU zafikia mkataba wa baada ya Brexit

Hata hivyo wakati makubaliano hayo yakikaribishwa mjini London na Brussels kama ukurasa mpya wa uhusiano baina yao, Ireland Kaskazini inasema bado yapo maswali yanayohitaji majibu. 

Ireland Kaskazini ni sehemu ndogo ya kisiwa cha Ireland, ambayo iko chini ya himaya ya Uingereza, wakati sehemu kubwa iliyobaki ya kisiwa hicho ikiwa jamhuri na mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Nordirland als geopolitischer Brennpunkt
Sehemu ya Ireland ya Kaskazini kati ya Jamhuri ya Ireland na UingerezaPicha: Ulrich Zillmann/FotoMedienService/picture alliance

Nafasi ya kufungua ukurasa mpya

Akiyazungumzia makubaliano hayo, Ursula von der Leyen alisema ni fahari kuona Uingereza na Umoja wa Ulaya wakitimiza ahadi waliyowekeana miezi kadhaa iliyopita, na kuelezea imani yake kuwa yataleta tija kwa watu wa pande zote mbili.

''Mfumo huu mpya unaturuhusu kufungua ukurasa mpya, na unatoa nafasi kwa suluhu ya kudumu ambayo tuna uhakika itawafaa watu wote na wafanyabiashara wa Ireland Kaskazini,'' alisema von der Leyen na kuongeza kuwa  ''ni suluhu inayojibu maswali yote waliyoyauliza.''

Soma zaidi: Wakazi wa Uingereza wajutia uamuzi wa Brexit

Mapya katika mfumo huo ni kwamba bidhaa zinazotoka sehemu nyingine za Uingereza kwenda Ireland Kaskazini pekee zitapita katika ukaguzi mwepesi ulioitwa ''ujia wa kijani'', huku zile ambazo zitashukiwa kuwa na uwezekano wa kupenya hadi Jamhuri ya Ireland, na kwa maana hiyo, katika eneo la soko huru la Umoja wa Ulaya, zitapita katika ukaguzi wa kina, ulioitwa ''ujia mwekundu'', chini ya sheria za Umoja wa Ulaya.

Nordirland | Brexit | Warentransport
Mfumo mpya uliosainiwa unaepusha vizuizi vikali kwa bidhaa kai ya Kisiwa kikuu cha Uingereza na Ireland ya KaskaziniPicha: Charles McQuillan/Getty Images

Hadhi ya Ireland Kaskazini katika Ufalme wa Uingereza

Kupitia mfumo huo ulioafikiwa, waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema serikali yake imeweza kuilinda hadhi ya Ireland Kaskazini ndani ya mfumo wa ufalme wa Uingereza.

''Kwanza, mfumo huu unawezesha mtiririko wa biashara usio na vikwazo ndani ya Uingereza. Bidhaa zinazokwenda Ireland Kaskazini zitapita katika ujia wa kijani, zikitengwa na zile zinazoweza kuingia katika Umoja wa Ulaya, na pili, tumelinda nafasi ya Ireland Kaskazini katika muungano wa Uingereza,'' amesema Waziri Mkuu Rishi Sunak.

Soma zaidi: Mkwamo wa Brexit waendelea kati ya EU na Uingereza

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema mahakama ya juu ya Umoja wa Ulaya itaendelea kuwa na kauli ya mwisho juu ya sheria zinazohusu Ireland Kaskazini, hali ambayo wachambuzi wanaamini itawaudhi wakaazi wa sehemu hiyo ya Uingereza, ambao walitaka kuachana kabisa na sheria za Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesafiri kwenda katika eneo hilo Jumanne, kujaribu kutuliza wasiwasi huo.

 

Vyanzo: rtre, afpe