1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brussels. Mawaziri wakutana kutayarisha mkutano wa wakuu wa umoja wa Ulaya.

5 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCM3

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels leo Jumatatu kutayarisha mkutano wa umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki hii.

Mawaziri hao wanamatumaini ya kupunguza tofauti baina ya mataifa wanachama kuhusiana na suala la nishati na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema kuwa ni muhimu kuwa umoja huo wenye wanachama 25 ukubaliane kuhusiana na malengo maalum ya kupunguza utoaji wa gesi za carbon zinazoharibu mazingira. Ujerumani ambayo inashikilia hivi sasa urais wa umoja wa Ulaya , inataka kupata ahadi kamili ya kupunguza utoaji wa gesi hizo kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020. Ujerumani pia inasisitiza kuongeza matumizi ya nishati mbadala kwa kiasi kama hicho. Mawaziri hao wa mambo ya kigeni pia wanatarajiwa kutoa wito wa kutoa vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran kwa kushindwa kufikia muda wa mwisho wa umoja wa mataifa wa kusitisha urutubishaji wa madini ya Uranium.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Luxemburg Jean Asselborn amesema kuwa njaa na magonjwa ya ukimwi yanasumbua watu wengi duniani na ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kupambana na tatizo hili.

O-Ton

Kwangu mimi naona haieleweki, kwamba hivi sasa baada ya kuuangusha ukuta , bado tunataka kuusimamisha tena. Kama mtu atafikiria ni kiasi gani cha fedha kinachohitajika , ili kupambana na njaa , na kama mtu atafahamu ni kiasi gani kombora moja linaweza kugharamia kufuta ugonjwa wa ukimwi katika Afrika, kwa hiyo jumuiya ya kimataifa inapaswa kufikiria kwa makini, ni wapi tumekwama.