1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yarejea kutifua vumbi

Bruce Amani
8 Januari 2018

Ligi Kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga inarejea tena kwa ajili ya mzunguko wa pili wa msimu, baada ya mapumziko mafupi ya kipindi cha barafu.

https://p.dw.com/p/2qWdL
TSG 1899 Hoffenheim v FC Schalke 04 - Bundesliga
Picha: Getty Images/A.Grimm

Bayern Munich ambao walikuwa na kambi ya mazoezi ya siku sita mjini Doha, Qatar na watashuka dimbani Ijumaa dhidi ya Bayer Leverkusen. Miamba hao wako kileleni mwa ligi na pengo la pointi 11 lakini bado kuna masuala kadhaa wanayostahili kuyashughulikia. 

Utafiti kuhusu VAR

Na wakati Bundesliga inarejea tena kutifua vumbi, suala jingine ambalo liliigubika nusu ya kwanza ya msimu ni mfumo wa mwamuzi msaidizi anayeanglia picha za video – VAR. Mechi nyingi tu zilikumbwa na maamuzi yenye utata. Na sasa karibu nusu ya wachezaji wa Bundesliga wamejitokeza kuupinga mfumo huo.

Katika uchunguzi uliochapishwa leo, na jarida la Kickerm asilimia 47 ya wachezaji walipinga mfumo huo ikilinganishwa na asilimia 42 ambao wanaunga mkono. Asilimia 11 hawakutoa maoni yao.

Jumla ya wachezaji 219 walishiriki katika uchunguzi huo wa kila nusu yam waka, na tena wakampigia mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski kuwa mchezaji bora. Kipa wa Schalke Ralf Faehrmann alipigiwa kura kuwa kipa bora wakati Leon Bailey wa Bayer Leverkusen akatambulika kuwa mchezaji bora aliyeingia katika ligi kwa mara ya kwanza.

Domenico Tedesco, katika msimu wake wa kwanza katika klabu ya Schalke, alipigiwa kura kuwa kocha bora kufikia sasa, wakati Pep Guardiola akiibuka mshindi kuwa kocha bora kabisa duniani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman