1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge jipya kukutana mara ya kwanza DRC

Lilian Mtono
28 Januari 2019

Baada ya Felix Tshisekedi kuapishwa rasmi kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hatua nyingine muhimu inayotarajiwa leo nchini Kongo ni kuidhinishwa kwa bunge jipya.

https://p.dw.com/p/3CJ3K
Demokratische Republik Kongo Kinshasa - Amtseinführung: Felix Tshisekedi wird Kongos Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Vuguvugu lililoundwa na rais aliendoka madarakani Joseph kabila linajivunia kunyakuwa asilimia 70 ya viti bungeni na kuwa na uwezekano wa kuteuwa waziri mkuu, huku chama chaTshisekedi kikiwa na asilimia kumi pekee ya viti bungeni.

Kikao cha kwanza cha bunge kitahusika na kuidhinisha mihula ya wabunge wote na pili kutunga kanuni za bunge. Mbunge mwenye umri mkubwa kuliko wote ndie atakaechukuwa nafasi ya spika hadi kuitishwa kwa uchaguzi wa spika mpya. Kwa sasa ni mpinzani Gabriel Kyungu wa Kumwanza mwenye umri wa miaka 81 kutoka mji wa Lubumbashi ambae ataliongoza kwa kipindi cha siku 60 baraza hilo la bunge.

Vuguvugu la upinzani la LAMUKA, la Martin Fayulu ambalo limeendelea kudai ushindi kwenye uchaguzi wa rais, linaelezea kwamba halitosusia vikao vya bunge. Christelle Vuanga, mbunge mteule wa jiji la Kinshasa kutoka upinzani ambae leo atahudhuria kwa mara ya kwanza kikao cha bunge amelezea msisimuko wake na dhamana kwa ajili ya raia waliompigia kura.

Alinukuliwa akisema ''Sasa hivi nimekuwa mwanasiasa na sio tena mwandishi habari kama nilivyokuwa hapo nyuma. Na ijapokuwa nimetokea upinzani lakini sitokubali misimamo ya kauli moja, kwa sababu kila mtu yuko huru kuelezea maoni yake na mimi nitafanya hivyo''.

DR Kongo  Kinshasa Vereidigung Präsident Felix Tshisekedi
Viguvugu la FCC la rais aliyeondoka Joseph Kabila lina uhakika na kutoa waziri mkuu wa taifa hilo kwa kuwa lina wingi wa viti bungeni.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

FCC, vuguvugu la rais aliyemaliza muda wake Joseph Kabila linaelezea kuwa na udhibiti wa bunge kwa kunyakuwa viti 350 miongoni mwa viti 500 bungeni. Kikatiba ni kwamba waziri mkuu lazima atoke kwenye chama ama vuguvugu lenye wingi wa viti bungeni.

Chama cha rais mpya Felix Tshisekedi na mshirika wake Vital Kamerhe vina wabunge wasiozidi hamsini. Tayari duru zinaelezea kwamba kutakuweko na ushirikano baina ya rais mpya na chama cha Kabila. Lakini naibu katibu mkuu wa UDPS, Rubens Mikindo amesema kwamba licha ya matokeo hayo, raia wasubiri mabadiliko na mageuzi ya kweli nchini.

Waziri mkuu anatarajiwa kuteuliwa baada ya bunge kuanza vikao vyake. Rais Tshisekedi alieleza kwamba serikali yake itajumuisha pande zote katika lengo la kukuza maridhiano ya kitaifa.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo

Mhariri: Grace Patricia Kabogo