1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Israel lavunjwa na kuitishwa uchaguzi mpya

Sylvia Mwehozi
30 Mei 2019

Israel inalazimika kufanya uchaguzi mwingine mpya mnamo mwezi Septemba mwaka huu, baada ya wabunge kupitisha hoja ya kulivunja bunge kufuatia Waziri mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kuunda serikali ya muungano.

https://p.dw.com/p/3JUb5
Israel | Knesset
Picha: Getty Images/AFP/G. Tibbon

Bunge la Israel Knesset jana lilipitisha kura 74 dhidi ya 45 za kuunga mkono hoja ya kuvunjwa kwake na kuitishwa uchaguzi utakaofanyika Septemba 17. Netanyahu ambaye ameiongoza Israel kwa muongo mmoja uliopita, alionekana kujipatia muhula wa nne madarakani lakini alishindwa kuafikiana na washirika wake na hususan juu ya muswada unaopendekeza ulinzi wa Netanyahu dhidi ya tuhuma za rushwa.

Kuliko kuachia jukumu hilo la kuunda serikali kwenda kwa mmoja wa mahasimu wake, chama cha Likud cha waziri mkuu Netanyahu kilionelea bora kuwasilisha hoja ya kuvunjwa bunge ili ufanyike uchaguzi mpya ambao unakuwa wa pili ndani ya mwaka huu. Netanyahu amesema taifa hilo linalazimika kuingia katika uchaguzi "ambao haukuhitajika" lakini anaamini chama chake kitaibuka na ushindi.

"Tutafanya uchaguzi wa mapema, na kampeni za wazi zitakazotupatia ushindi. Tutashinda!, tutashinda na umma utashinda. Ni vigumu kuamini kwamba  Avigdor Lieberman sasa yuko upande wa kushoto. Avigdor Lieberman yuko upande wa kushoto.!", alisema kiongozi huyo. 

Israel Ministerpräsident Benjamin Netanjah in Jerusalem
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: picture-alliance/dpa/G. Tibbon

Kama muda wa mwisho ungepita ambao ulikuwa ni usiku wa saa sita bila ya kura kupigwa, rais wa Israel angeamua kumteua mbunge yeyote, ambaye alionekana kuwa kiongozi wa upinzani Benny Gants fursa ya kuunda serikali ya muungano. Mara tu baada ya kura kupigwa, Gants alimshutumu Netanyahu kwa kuamua kujilinda yeye mwenyewe badala ya kujali ya maslahi ya nchi.

Nchi hiyo sasa inaingia katika kampeni za uchaguzi mpya ambazo zitadumu angalau kwa miezi mitatu chini ya sheria ya Israel. Netanyahu amekuwa na mazungumzo ya takribani wiki sita bila ya mafanikio na chama cha waziri wa zamani wa ulinzi Avigdor Lieberman cha Yisrael Beiteinu na kile cha Kiyahudi cha Utra-Orthodox.

Soma zaidi ...

Hata akishinda uchaguzi ujao bado uwezekano wa kuunda serikali ya muungano ni mdogo na hivyo kulazimika kukubaliana na matakwa ya kisiasa ili kuungwa mkono yatakayomlazimu kusimama mahakamani kwa tuhma za rushwa. Mzizi wa fitina safari umetuama katika mvutano wa muda mrefu kati ya chama cha Yisrael Beiteinu na wafuasi wa itikadi kali za kidini-kuhusu kutoruhusiwa wanafunzi wa Talmud kutumikika jeshini.

Mkwamo huo wa kisiasa unaweza pia kuleta athari kwa juhudi za Marekani za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Tayari Marekani ilikwisha panga mkutano wa mwezi ujao nchini Bahrain kwa ajili ya kubainisha kile ilichokilelezea kuwa awamu ya kwanza ya mpango wake wa amani.