1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Marekani lachunguza udukuzi dhidi ya Urusi

Sekione Kitojo
5 Januari 2017

Maafisa waandamizi wa mashirika ya upelelezi nchini Marekani wako katika kikao cha mahojiano kwa ajili ya tathmini ya  vyombo vyao kwamba Urusi ilifanya udukuzi katika uchaguzi wa rais na kumsaidia Donald Trump kushinda.

https://p.dw.com/p/2VJuX
Washington Russische Botschaft
Ubalozi wa Urusi MarekaniPicha: picture-alliance/AA/Y. Ozturk

Kikao cha mahojiano  cha  kamati  ya huduma  za  majeshi  ya  taifa kuhusu  kitisho mtandaoni  leo Alhamis  kinakuja  siku  moja  kabla ya  rais  mteule  wa  Marekani Donald Trump  akitarajiwa kupewa taarifa  na  wakurugenzi  wa  mashirika  ya  ujasusi  CIA  na  lile  la uchunguzi  wa  makosa  ya  jinai FBI, pamoja  na  mkurugenzi wa usalama  wa  taifa, kuhusiana  na  uchunguzi  juu  ya  madai  ya udukuzi uliofanywa  na  Urusi.

Trump  amekuwa  akikosoa  sana  ugunduzi  wao, hata  kuonekana kuunga  mkono mtazamo  wa  mwanzilishi  wa  tovuti  inayofichua masuala  ya  siri za  serikali  Julian Assange  kwamba  Urusi haikumpa barua  pepe  za  chama  cha  Democratic  zilizodukuliwa.

US-National Intelligence Director James Clapper
Mkurugenzi wa usalama wa taifa nchini Marekani James ClapperPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Lakini msemaji  wa  Ikulu  ya  Marekani  ya  White House, Josh Earnest  amesema tathmini  iliyotolewa  kwa  pamoja  na  vyombo vya  upelelezi inaonesha  wazi  kuwa Urusi  ilikuwa  ikiingilia  shughuli za  uchaguzi  nchini  Marekani.

"Tarifa hiyo ambayo  ilitolewa  na  vyombo  vya  upelelezi Oktoba mwaka  2016  kabla  ya  uchaguzi inaweka  wazi kwamba  Urusi ilikuwa  inaingilia  kati  katika  uchaguzi  wetu na kuwalikisha mtazamo  wa  pamoja  wa  mashirika  17 tofauti  ya  upelelezi. Hii  si kawaida  ya vyombo  hivi  kufanya  kazi. Hali  ya mawazo yanayolingana, hususan hali  ikiwa  ya  mvutano, ni  suala la kutafakari. Uamuzi  wa  vyombo  vya  upelelezi, sio tu  kufikia hitimisho  lakini kuiweka  wazi ripoti  yao, ni  jambo  kubwa  na nafikiri inaakisi kina cha hali  yao  ya  kuamini tathmini  yao."

Kujitayarisha kwa mashambulizi yajayo

Kikao  hicho  cha  kamati  ni  cha  kwanza  katika  mfululizo  wenye lengo  la  kufanya  uchunguzi  juu  ya  kile  kinachofikiriwa  kuwa  ni mashambulizi  ya  mtandaoni  yaliyofanywa  na  Urusi  dhidi  ya maslahi  ya  Marekani  na  kutengeneza  ulinzi imara  wa  kutosha kuhusu  uingiliaji  katika  siku  zijazo.

Symbolbild Wikileaks Enthüllungen
Udukuzi wa mtandaoni ni madai yanayotolewa na Marekani dhidi ya UrusiPicha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Shutuma  za  Urusi  kuingilia  katika  uchaguzi  wa  mwaka  2016 kwa kudukua kurasa  za  barua  pepe  za  chama  cha  Democratic zimeizunguka  serikali  mjini  Washington  kwa  wiki  kadhaa. Rais Barack Obama  alilipiza  kwa  Urusi  mwishoni  mwa  mwezi Desemba  kwa  kuchukua  hatua  ya  kuweka  vikwazo vinavyolenga mashirika  ya  ujasusi  ya  Urusi, lile  la  GRU  na  FSB, ambayo Marekani  ilisema  yanahusika.  GRU ni  shirika  la  Urusi linaloshughulika  na  masuala  ya  ujasusi  wa  kijeshi. Lile  la FSB ni mrithi  wa  shirika  la  wakati  wa  enzi  za  Umoja  wa  Kisovieti  la KGB.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo