1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uingereza laukataa mpango wa May kuhusu Brexit

Grace Kabogo
13 Machi 2019

Wabunge wa Uingereza wamepiga kura kuupinga mpango wa Waziri Mkuu, Theresa May wa nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit.

https://p.dw.com/p/3EuUI
Großbritanien | Theresa May spricht im Unterhaus | Brexit | London
Picha: Reuters/UK Parliament/J. Taylor

Wabunge 391 wamepiga kura ya hapana, huku 242 wakipiga kura kuunga mkono mpango huo uliofikiwa kati ya May na Umoja wa Ulaya. Mwezi Januari mpango wa May ulipingwa kwa kura 230.

Kabla ya kura hiyo May alipata hakikisho la mabadiliko ya kisheria kuhusu mpaka wa Ireland katika juhudi za kuwashawishi wabunge kuunga mkono mpango wake. Uingereza inatarajiwa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya Machi 29. Mapema jana Mwanasheria Mkuu wa Uingereza, Geoffrey Cox alisema ufafanuzi kuhusu mabadiliko hayo yanapunguza tu hatari kuhusu Uingereza kuendelea kunasa katika sheria za Umoja wa Ulaya, lakini hayaondoi kabisa uwezekano huo.

Baada ya kura hiyo, Theresa May aliwaonya wabunge kwamba haitokuwa rahisi kuongeza muda wa mazungumzo ya mchakato wa Brexit na Umoja wa Ulaya. Amebainisha kuwa kitakachofuata sasa ni kura ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya bila ya kufikiwa kwa makubaliano ambayo itapigwa leo.

Matatizo hayatotatuliwa kwa kuchelewa kuondoka

May amefafanua kuwa kura ya kuondoka bila ya makubaliano au kuchelewesha muda wa kuondoka, haitayatatua matatizo yaliyopo. Amesema kama hilo ndilo litakuwa chaguo, kesho Alhamisi wabunge wataamua iwapo waongeze muda wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, ameonya kuwa Umoja wa Ulaya utahitaji sababu ili uweze kuliidhinisha suala hilo.

Kiongozi wa kampeni ya Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya, Nigel Farage amesema matokeo ya kura hiyo yameonyesha kushindwa vibaya kwa uongozi wa May. Naye kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn amesema May sasa anapaswa kukiri kwamba mkakati wa serikali yake umeshindwa.

Großbritanien | Brexit | London
Waandamanaji wakiwa nje ya bunge la UingerezaPicha: picture-alliance/dpa/AP/T. Ireland

Mamia ya waandamanaji kutoka kambi pinzani walishangilia nje ya bunge la Uingereza, ambapo waliungana kuupinga mpango wa May uliokataliwa na bunge, lakini walitofautiana kuhusu maana ya hatua hiyo.

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na nchi 27 wanachama wa umoja huo wameonya katika taarifa ya pamoja kwamba hatua ya wabunge wa Uingereza kuukataa mpango wa May, imeongeza uwezekano mkubwa wa kuwepo Brexit isiyo na makubaliano.

Maas aishutumu Uingereza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema uamuzi huo wa bunge unaashiria kuwa wanakaribia kuwa na Brexit isiyo na makubaliano. Maas ameishutumu Uingereza kwa kucheza kamari bila kujali ustawi wa wananchi na uchumi. Ameongeza kusema kuwa Uingereza na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuzingatia jinsi ya kuangalia mustakabali wa uhusiano wao, baada ya Brexit.

Mwakilishi wa bunge la Umoja wa Ulaya anayesimamia mchakato wa Brexit, Guy Verhofstadt, amesema pande zote nchini Uingereza zinahitaji kupata makubaliano ya kitaifa kuhusu Brexit ili iweze kuutatua mzozo uliopo sasa. Amesema iwapo hilo litafanikiwa, basi watashiriki kikamilifu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, amesema kwamba amesikitishwa na matokeo ya kura hiyo. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Uingereza inahitaji kuwa na ushawishi madhubuti iwapo itapiga kura kuongeza muda wa Brexit, hivyo kutoa muda zaidi wa kufanyika mazungumzo.