1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani laidhinisha bajeti ya ziada ya mwaka 2023

Daniel Gakuba
15 Desemba 2023

Bunge la Ujerumani, Bundestag limeidhinisha bajeti ya nyongeza ya serikali kwa mwaka 2023, baada ya kulazimika kuondoa kwa muda kanuni ya ukomo wa kukopa.

https://p.dw.com/p/4aDxw
Bunge la Ujerumani, Bundestag
Ukumbi wa Bunge la Ujerumani mjini BerlinPicha: Annegret Hilse´/REUTERS

Bajeti ya Ujerumani ilitumbukia katika mzozo katikati mwa mwezi Novemba, baada ya mahakama ya katiba kuizuia serikali kutumia fungu la fedha zilizokuwa katika fuko maalumu la kupambana na janga la Covid-19.

Hatua hiyo ya bunge imefuatia wiki kadhaa za majadiliano baada ya uamuzi wa kushtukiza wa mahakama ya katiba, uliozuia matumizi ya euro bilioni 60 kutoka fuko la dharura kwa ajili ya kupambana na virusi vya corona.

Serikali ilitarajia kutumia fedha hizo katika mipango ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, sekta ambayo inatoa fursa nyingi za matumizi.

Mapema wiki hii serikali ya mseto  wa vyama vitatu inayoongozwa na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ilifikia makubaliano juu ya matumizi kwa mwaka 2024, ambayo yanaambatana na hatua kali za kubana matumizi.

Maumivu makali bei za nishati majumbani na vyombo vya moto

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani.
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani.Picha: Liesa Johannssen/REUTERS

Bajeti ya nyongeza iliyokubaliwa leo bungeni itagharimiwa na ongezeko la kodi juu ya utoaji wa hewa ya ukaa, ambayo makali yake yatasikika kupitia bei ya mafuta ya petroli na ya gesi ya kupasha joto majumbani.

Kodi hiyo ambayo leo hii ni euro 30 kwa kila tani moja ya hewa ya ukaa inayotolewa, itapanda hadi euro 45 kwa kila tani ya hewa ya ukaa mwaka 2024, badala ya euro 40 kama ilivyokuwa katika makadirio ya awali.

Kwa hali hiyo wenye magari watalipa senti 4.5 zaidi za euro kwa kila lita ya petroli, na kupitia ongezeko hilo litaiingizia serikali kipato cha takribani euro bilioni moja.

Kama sehemu ya mpango wa serikali ya mseto kuupatia ufumbuzi mzozo wa bajeti, wabunge walilazimika kuondoa kanuni nyingine juu ya sheria ya kukopa, ili kuweza kufidia matumizi ya siku za nyuma, zikiwemo fedha zilizotolewa kama ruzuku ya unafuu kwa wanunuzi wa bidhaa na huduma mbali mbali.

Hii ni mara ya nne mfululizo ambapo bunge la Ujerumani limelazimikwa kukwepa kanuni kali za ukomo wa serikali kukopa.

Je, serikali ya Scholz itaheshimu kanuni ya mikopo mwaka ujao?

Tamasha la nishati jadidifu mjini Hamburg
Serikali ya Ujerumani ilihitaji fedha ziada kufadhili miradi ya nishati jadidifu.Picha: Chris Emil Janflen/imago

Ujerumani huwa inachukua tahadhari kubwa katika kudhibiti ukubwa wa deni la serikali.

Sheria ya nchi hii huiruhusu serikali kukopa tu wakati wa majanga ya kimaumbile, au wakati wa dharura ambayo iko nje ya uwezo wa serikali, na mabayo inaweza kuathiri pakubwa hali ya kifedha.

Serikali ya Kansela Scholz imetetea ukopaji inaoufanya kwa kutoa sababu mbali mbali, zikiwemo ongezeko kubwa la bei ya nishati litokanalo na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na juhudi za kujenga upya miundombinu iliyoharibika katika mafuriko ya mwaka 2021 magharibi mwa Ujerumani.

Deni jipya la serikali linakadiriwa kufikia euro bilioni 70.61, ikimaanisha ongezeko la euro bilioni 44.8 juu ya kiwango kinachoruhusiwa.