1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Bunge la Ulaya lapitisha mageuzi ya sera ya uhamiaji

11 Aprili 2024

Bunge la Umoja wa Ulaya limepitisha mageuzi makubwa ya sera za waomba hifadhi ambazo zitaimarisha taratibu za mipakani na kulazimisha mataifa yote 27 ya umoja huo kugawana majukumu.

https://p.dw.com/p/4eeaP
Bunge la Ulaya
Wabunge wa Bunge la Ulaya wanashiriki katika msururu wa kura wanapohudhuria kikao cha mashauriano katika Bunge la Ulaya mjini Brussels.Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Vikundi vikuu vya kisiasa vya bunge vilishinda upinzani kutoka kwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na za mrengo mkali wa kushoto ili kupitisha mageuzi hayo.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesifu mageuzi hayo, akisema yatalinda mipaka ya Ulaya na kuhakikisha ulinzi wa haki za msingi kwa wahamiaji.

Soma pia: Bunge la Ulaya kupigia kura marekebisho ya sheria za waomba hifadhi

Kiongozi huyo ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya ndio unapaswa kuamua nani wa kuingia Ulaya na kwa mazingira gani lakini sio walanguzi na wasafirishaji haramu wa binadamu.

"Hivi ndivyo mkataba wa uhamiaji na waomba hifadhi utafanya kazi, utaleta mabadiliko ya kweli kwa raia wote wa Ulaya. Kwanza, mipaka ya Ulaya iliyo salama zaidi, kujua hasa ni nani anayevuka mipaka yetu kwa kusajili na kuchunguza kila mtu, kwa kuhakikisha ulinzi wa haki za msingi kwa njia ya ufuatiliaji wa kujitegemea."

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na waziri wa uhamiaji wa Ugiriki, Dimitris Kairidis, wote wameitaja kura hiyo kuwa ya kihistoria.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amepongeza mageuzi hayo akisema Ulaya inafanya kazi kwa kile alichokitaja kuwa "ufanisi na ubinadamu" huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia Matteo Piantedosi akipongeza kwamba ni "maelewano bora zaidi".

"Haki za binaadamu zitakiukwa" Wakosoaji

Maandamano nje ya Bunge la Ulaya- Sera ya Uhamiaji
Wanaharakati waandamana kupinga mkataba wa uhamiaji nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya, Brussels Ubelgiji.Picha: Johanna Geron/REUTERS

Kwa kuzingatia sababu mbalimbali mashirika ya misaada ya wahamiaji pia yalikashifu mkataba huo.

Shirika la kimatiafa la kutetea haki za binadamu la Amnesty, limekosoa makubaliano hayo iliyoyataja kama "ya aibu" na kwamba Umoja wa Ulaya unaunga mkono makubaliano ambayo "wanayojua yatasababisha mateso makubwa zaidi ya binadamu."

Johannes Rueckeel msemaji wa shirika la wahamiaji la Seebrücke anasema "Tunapinga mkataba huu wa uhamiaji kwa sababu hakuna kitakachoboreshwa na mambo yatakuwa mabaya zaidi, haki za binadamu zitawekewa vikwazo. Watu wataingizwa katika hatari zaidi."

Shirika la Msalaba Mwekundu limezitaka nchi wanachama kuhakikisha hali ya kibinadamu kwa wanaotafuta hifadhi na wahamiaji walioathirika zinalindwa.

Kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa, Marine Le Pen, alilalamika kuwa mabadiliko hayo yatatoa kile alichokitaja kama "kutokuadhibiwa kisheria kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayohusika na wasafirishaji haramu."

Hatua za mkataba huo zitaanza kutumika mwaka 2026, baada ya Halmashauri Kuu ya Ulaya kueleza kwa mara ya kwanza jinsi utakavyotekelezwa.