1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBurkina Faso

Burkina Faso yasitisha matangazo ya redio ya BBC na VOA

26 Aprili 2024

Baraza la mawasiliano la Burkina Faso limeamuru watoa huduma za mtandao kusimamisha ufikiaji wa tovuti na majukwaa mengine ya kidijitali ya BBC, VOA na shirika la Human Rights Watch, HRW

https://p.dw.com/p/4fEmQ
Nembo ya shirikala kutetea haki za binadamu
Nembo ya shirikala kutetea haki za binadamuPicha: John MacDougall/AFP/Getty Images

 

Burkina Faso imesimamisha matangazo ya redio ya Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC Afrika na lile linalofadhiliwa na Marekani la Voice of America, VOA, kwa muda wa wiki mbili kutokana na matangazo walioyapeperusha ikilishutumu jeshi kwa mauaji ya kiholela.

Soma zaidi. HRW: Vikosi vya jeshi Burkina Faso vimewauwa raia 223

Baraza la mawasiliano la Burkina Faso limesema kupitia taarifa yake kwamba wameamuru watoa huduma za mtandao kusimamisha ufikiaji wa tovuti na majukwaa mengine ya kidijitali ya BBC, VOA na Shirika la kimataifa la utetea haki za binadamu, Human Rights Watch, HRW kutokana na kutangaza taarifa hiyo.

Uchunguzi wa shirika la Human Rights Watch

Ripoti hiyo ya shirika la HRW imeeleza kuwa jeshi limetekeleza ukatili dhidi ya raia kwa kisingizo cha kupambana na ugaidi.

Kulingana na uchunguzi wa shirika hilo, mwezi Februari jeshi la nchi hiyo ya Afrika Magharibi liliwauwa wanakijiji wapatao 223, wakiwemo watoto 56, kama sehemu ya kampeni dhidi ya raia wanaoshutumiwa kushirikiana na wanamgambo wa jihadi.

Picha ya vlogger wa Kiafrika
Picha ya vlogger wa Kiafrika akitumia maikrofoni kwa mazungumzo na waliojisajili kwenye podikasti ya mitandao ya kijamiiPicha: YAY Images/IMAGO

Shirika la HRW lilisema jeshi la Burkinabe lilifanya ukatili huo dhidi ya raia mara kadhaa na ilitoa wito kwa mamlaka kuchunguza mauaji hayo.

Soma zaidi. Amnesty: Haki za binadamu duniani zinakabiliwa na vitisho

Hata hivyo, baraza la mawasiliano la Burkina Faso limeitaja ripoti ya hiyo ya HRW kama yenye matamshi yenye utata na yasio na umakini, dhidi ya jeshi, hali inayoweza kuleta machafuko ya umma, hivyo inasitisha matangazo ya mashirika hayo, kutokana na kuitangaza habari hiyo.Amnesty: Haki za binadamu duniani zinakabiliwa na vitisho

VOA yasisitiza inazingatia maadili ya uandishi wa habari

"VOA inashikilia msimamo wake kuhusu uamuzi wa kuripoti taarifa hiyo kuhusu Burkina Faso na inakusudia kuendelea kuangazia kikamilifu na kwa haki matukio katika nchi hiyo," alisema Kaimu Mkurugenzi wa VOA John Lippman. Lippman alisema Sauti ya Amerika inafuata kikamilifu kanuni za uandishi wa habari sahihi, wenye uwiano, na wa kina, kwa hiyo, wanaisihi serikali ya Burkina Faso kufikiria upya uamuzi huo.

Burkina Faso - Polisi wa Burkina Faso
Burkina Faso - Polisi wa Burkina Faso wanaweka kizuizi mnamo Agosti 14, 2017 huko Ouagadougou, kufuatia shambulio baya la watu wenye silaha kwenye mkahawaPicha: Ahmed Ouoba/AFP/Getty Images

HRW ilifanya uchunguzi wake baada ya mwendesha mashtaka kusema mnamo mwezi Machi kuwa takribani watu 170 waliuawa na washambuliaji wasiojulikana wakati wa mashambulizi kwenye vijiji vya Komsilga, Nondin na Soro.

Hali ya mapinduzi katika mataifa ya Sahel

Burkina Faso ni mojawapo ya mataifa ya Sahel ambayo yamekuwa yakipambana kuzuia uasi wa makundi yenye itikadi kali za Kiislamu yanayohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu ambayo yameenea kutoka nchi jirani ya Mali tangu mwaka 2012, na kuwaua maelfu ya watu na wengine mamilioni kuyakimbia makazi yao.

Soma zaidi. 

Masaibu ya waandishi habari wa Kongo

Hali ya kukatishwa tamaa kutokana na mamlaka kushindwa kuwalinda raia katika ukanda wa Sahel, kumechangia mapinduzi yaliyofanyika mara mbili nchini Mali, mara mbili Burkina Faso na mara moja nchini Niger tangu mwaka 2020.

"Tumesikitishwa sana na taarifa za mauaji ya idadi kubwa ya raia, wakiwemo watoto... katika mapigano kati ya vikundi vyenye silaha na vikosi vya majeshi vya Burkinabe," ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa yake.

AFP, AP, Reuters