1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BVB yaibuka kidedea dhidi ya mahasimu wao wa jadi Schalke

Sekione Kitojo
10 Desemba 2018

Borussia  Dortmund  yaibuka  kidedea  pambano  la  watani  wa  jadi Derby , dhidi  ya Schalke 04, Bayern  nayo  yajitutumua kuifukuzia Dortmund.

https://p.dw.com/p/39onH
FC Schalke 04 - Borussia Dortmund
Picha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

Katika  Bundesliga  nusu  ya  pili  ya  mwaka  huu  2018  katika  soka la  Ujerumani  inamilikiwa  bila  shaka  na  Borussia  Dortmund. Katika  mchezo  wa  14  kati ya  michezo  17  ya  duru  hii  ya kwanza  mashati  ya  BVB  yameendelea  kubakia  safi bila  doa.

Imeshinda  mara  11  na  sare  tatu, na  bila  kushindwa. Washambuliaji  wa  BVB wameendelea  kupata  mabao  na  wana kiwango  bora  katika  ligi  hadi  sasa , wakipachika  wavuni  mabao 39, ambapo Paco Alcacer, Marco Reus na  wengine wamezisalimia nyavu  za  timu  pinzani  bila  kusita.

1. Bundesliga | Schalke 04 v Borussia Dortmund | Torjubel (1:2)
Mshambuliaji chipukizi Jadon Sancho wa Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa/I. Fassbender

Kocha  Lucien Favre  ameweza kuunda  kikosi  imara  katika  muda  wa  nusu  mwaka , ambacho kinauhakika  wa  kuwa  bingwa  wa  majira  ya mapukutiko na  hata kumaliza  kipindi  hiki  ikiwa  kileleni  mwa   msimamo  wa  ligi.

Borussia  Dortmund  ilifanikiwa  kuangusha  Schalke  04  mahasimu wao  wa  jadi  katika  mpambano  wao  siku  ya  Jumamosi  kwa mabao  2-1, ukiwa ni  ushindi  wao  wa  kwanza  katika  muda  wa misimu  mitano. Borussia  Dortmund  haijashinda   katika  mpambano huu  wa  watani  wa  jadi  dhidi ya  Schalke  tangu  Novemba  mwaka 2015  ambapo  kutwaa  ushindi  wa  mabao 3-2.

Mara  zote Schalke wamekuwa  washindi  ama  timu  hizo  kutoka  sare. Dortmund imeshinda  mara  33  hadi  sasa  kati  ya  michuano  93  ya Bundesliga  dhidi  ya  Schalke 04  wakati  Schalke  imeshinda  mara 31, na   timu  hizi  mbili  zimetoka  sare  mara 29. Schalke  sasa inatofautiana  na  mahasimu  wao  hao  wa Dortmund  kwa  pointi 22.

1. Bundesliga | Schalke 04 v Borussia Dortmund
Wachezaji wa Schalke 04 wakitoka uwanjani vichwa chiniPicha: Reuters/L. Kuegeler

Borussia Moenchengladbach yapanda

Borussia  Moenchengladbach  imepanda  hadi  nafasi  ya  pili  katika Bundesliga  jana  Jumapili  baada  ya  kupata  ushindi  wa  mabao 3-0  dhidi  ya  Stuttgart na  katika  mchezo  wa  kwanza  Mainz  ilitoka sare  ya  bao 1-1  na  Hannover  96. Gladbach  imeiondoa  Bayern Munich  katika  nafasi  ya  pili  ya  msimamo  wa  ligi  baada  ya ushindi  huo na  kocha  wa  Gladbach Dieter  Hecking  aliwaambia waandishi  habari  za  michezo  kuwa "tunajiamini  tukiwa  nyumbani," na  kuongeza  kwamba  "katika  kipindi  cha  pili nilichukua  hatua  ya kucheza  kamari  kidogo kwa  matumaini  ya  kuongeza  kiwango cha kasi.   Nguvu  ya  kikosi  kilichoko  katika  benchi ni  kitu  ambacho hatukuwa  nacho  msimu  uliopita."

Fußball Bundesliga Borussia Mönchengladbach vs. VfB Stuttgart
Wachezaji wa Borussia Moenchengladbach wakipambana na wachezaji wa VFB Stuttgart na kupata ushindi wa mabao 3-0Picha: picture-alliance/dpa/C. Müller

Ushindi  huo wa  saba  wa  Gladbach  katika  michezo  saba  ya nyumbani  msimu  huu  umeiweka  timu  hiyo  juu  ya  bayern  na sasa  wanaifuta  Dortmund  nyuma  kwa  pointi  saba.

Timu zinazowania  kucheza  katika  vikombe  vya  Ulaya , kombe  la mabingwa  Champions  League  na  Ligi  ya  Ulaya  Europa  League ni  pamoja  na  RB Leipzig  iliyoko  katika  nafasi  ya  4, ikiwa  na pointi 25, licha  ya  kufungwa  mabao 3-0  na  Freiburg, wakati Freiburg  imejisogeza  hadi  nafasi  ya  12.

Deutschland 1. FSV Mainz 05 v Hannover 96 - Bundesliga | Tor Hendrik Weydandt
Wachezaji wa Hannover 96 wenye sare za kijani wakishangiria bao dhidi ya Mainz 05Picha: Getty Images/Bongarts/S. Hofmann

Eintracht  Frankfurt  iko katika  nafasi  ya  5  ikiwa  na  pointi 23 licha  ya  kufungwa  bao 1-0 na  Hertha  Berlin  ambayo  nayo  iko  katika  nafasi  ya  6.

Fortuna Dusseldorf , Hannover 96  na  VFB Stuttgart ziko  katika nafasi  za  kushuka  daraja, nafasi  za  16, 17  na  18.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape / dpae / rtre / afpe

Mhariri:  Yusuf Saumu