1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema chatoa shutma kali kwa rais wa Tanzania Samia Suluhu

Amina Mjahid
17 Mei 2022

Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, kimemshtumu rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusika katika kuwarudisha bungeni, wabunge 19 wa viti maalum wa chama hicho ambao walifutiwa uanachama.

https://p.dw.com/p/4BPBv
Samia Hassan | Präsidentin von Tansania
Picha: Hannah Mckay/AFP/Getty Images

Siku chache baada ya Spika wa Bunge Tulia Ackson, kutangaza kuwaruhusu wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila, amesema kinachofanyika ni uvunjifu wa Katiba na Sheria, ulioanzishwa na Hayati John Magufuli na sasa unaendelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kigaila amesema wapo tayari kuendelea na kesi hiyo mahakamani kwa sababu hawajawahi kushindwa kesi. Kadhalika katika mkutano huo, Kigaila alitumia zaidi ya saa moja kueleza mchakato wa kinidhamu uliofanywa na chama hicho kwa wabunge hao, kuanzia maamuzi ya kamati kuu, hadi juzi Mei 12 walipowahoji na hatimaye Baraza Kuu kuridhia kuwavua uanachama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mrema alisema, kinachoendelea ni kwa wabunge hao kuendelea kulipwa mishahara hewa kwa sababu hawatambuliki na wapo bungeni kinyume cha sheria.

Haya yanajiri wakati mkutano kati ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Rais Samia Suluhu Hassan, ukitarajiwa kufanyika siku za usoni, hali ambayo inaleta ombwe la  maridhiano ya kisiasa nchini Tanzania.

Mwandishi: Florence Majani. DW