1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama Kikuu cha upinzani SPD kujiunga na serikali ya mseto

Abdu Said Mtullya14 Desemba 2013

Chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani Social Demokratik,SPD kimegiga kura ya kujiunga na serikali ya mseto na vyama vya kihafidhina ,CDU na CSU.

https://p.dw.com/p/1AZja
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akifurahia kupitishwa kwa mkataba wa serikali ya mseto.
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akifurahia kupitishwa kwa mkataba wa serikali ya mseto.Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Mweka hazina wa chama cha SPD Barbara Hendricks ametoa taarifa hiyo baada ya kura zaidi ya 300,000 kuhesabiwa za wanachama waliopiga kura kuunga mkono mkataba wa serikali ya mseto ya vyama vikuu.

Baada ya miezi mitatu tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa nchini Ujerumani, wanachama 475,000 wa chama kikuu cha upinzani Social Demokratik bado walikuwa wanajadiliana iwapo kujiunga na serikali hiyo.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho hapo awali walishaashiria uwezekano makubwa juu ya wanachama wao kuunga mkono mkataba wa kuunda serikali ya mseto .

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel amewaambia wanachama wa chama hicho kwamba kujiunga na serikali ya mseto kutakuwa na manufaa makubwa kwa chama chao. Ametahadharisha kuwa ,kutojiunga na serikali hiyo kungeweza kusababisha maonevu zaidi ya kijamii kwa mamilioni ya watu nchini Ujerumani. Hata hivyo Bwana Gabriel amekiri kuwa kujenga mfungamano na vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na Kansela Angela Merkel siyo mshikamano wa hiari bali unatokana na kutambua hali halisi.

Wakati huo huo baadhi ya vyombo vya habari vimeshadokezea juu ya baraza la mawaziri linalotarajiwa kuundwa. Kwa mujibu wa vyombo hivyo Waziri wa fedha wa hadi sasa Wolfgang Schäuble ataendelea na wadhifa huo. Waziri Schäuble anazingatiwa kuwa nguzo kuu mojawapo iliyosimama imara katika kuukabili mgogoro wa fedha barani Ulaya.

Wolfgang Schäuble Steuerschätzung
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: picture-alliance/dpa

Vyombo vya habari pia vimedokezea kwamba Waziri wa ulinzi Thomas de Maizere pia ataendelea kuitumikia wizara hiyo.

Na katika upande wa chama kikuu cha upinzani ,Social Demokratik watakaokuwamo katika baraza jipya la mawaziri ni Bwana Frank-Walter Steinmeier anaetarajiwa kuwa waziri wa mambo ya nje. Bwana Steinmeier alishawahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani kuanzia mwaka wa 2005 hadi mwaka wa 2009.

Plagiatsvorwürfe gegen Frank-Walter Steinmeier SOCIAL MEDIA
Kiongozi wa wabunge wa SPD,Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel anatarajiwa kuiongoza inayoitwa Wizara Kuu,ya uchumi na ya mageuzi ya nishati. Bwana Gabriel atausimamia mchakato wa kuondokana na matumizi ya nishati ya nyuklia na badala yake kuelekea kwenye nishati mbadala.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo mwezi wa Septemba chama cha Kansela Angela Merkel CDU kilipata asilimia 41.5 ya kura na hivyo kushindwa kukifikia kiwango cha kuweza kuunda serikali peke yake. Katika uchaguzi huo chama cha Social Demokratik kilipata asilimia 25.7 tu ya kura, matokeo yanayozingatiwa kuwa mabaya kabisa kwa chama hicho, tokea kumalizika kwa vita kuu vya pili.

Mwandishi:Mtullya Abdu./dpa,ZA.
Mhariri: Mohamed Dahman