1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Burundi chashinda ubunge

8 Julai 2015

Chama tawala nchini Burundi CNDD FDD kimeshinda viti vingi vya bunge katika uchaguzi ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani. Kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini Burundi CENI, CNDD FDD kimeshinda.

https://p.dw.com/p/1Fv1v
Burundi Wahlen
Rais wa Tume huru ya uchaguzi Burundi, Pierre Clave NdayicariyePicha: picture-alliance/AP Photo/G. Ngingo

Chama tawala nchini Burundi CNDD FDD kimeshinda viti vingi vya bunge katika uchaguzi ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani. Kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini Burundi CENI, CNDD FDD kimeshinda viti 77 kati ya 100 vya bunge.

Mwenyekiti wa CENI Pierre Claver Ndayicariye aliyeyatangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika tarehe 29 mwezi Juni amesema muungano wa vyama vya upinzani ujulikanao Amizero y'Abarundi unaoongozwa na Agathon Rwasa ukipata viti 21. Uprona mshirika wa serikali kimepata viti viwili. na kuongeza idadi ya wapiga kura waliojitokea ilikuwa ni asilimia 74.32

FNL chama kinachoongozwa na Jacques Bigirimana pia mshirika wa serikali kimepata pigo kubwa kwa kutopata kiti hata kimoja hali kadhalika muungano Copa unaoongozwa na Jean De Dieu Mutabasi umeambulia patupu.

Kukiukwa kwa mkataba wa Arusha

Kwa mujibu wa katiba ya Burundi na mkataba wa Arusha matokeo hayo ni kinyume na sheria kwani hayajaheshimu usawa wa makabila ya Burundi na kijinsia unao agizwa kuwepo Burundi.

Parlamentswahlen in Burundi Wahllokal Wahlhelfer Wahlbeteiligung
Wasimamizi wa uchaguzi mjini BujumburaPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Hata hivyo changamoto iliyopo katika ugavi huo wa viti bungeni ni kuwa muungano wa Amizero ya Abarundi unao undwa na FNL ya Agathon Rwasa na Uprona ya Charles Nditije ulopata nafasi ya pili kwa viti 21, haujakubaliana na matokeo hayo ya uchaguzi waliosusia.

Tayari tume ya uchaguzi Ceni imeanzisha mashauriano Jumatano hii na vyama vya kisiasa vilivyopata viti bungeni ili kufikia uteuzi wa wabunge 18 wa kabila la watutsi na hivo kuleta usawa ili bunge liundwe kwa asilimia 60 wahutu, na 40 watutsi pamoja na asilimia 30 wanawake kwa mujibu wa katiba.

Hayo yanakuja wakati serikali ya Burundi na maafisa wa tume ya uchaguzi wakitarajiwa kukutana hii leo kuyajadili mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Tanzania Jumatatu hii ya kutaka uchaguzi wa Rais unaotarajiwa Jumatano ijayo kuahirishwa kwa majuma mawili.

Chini ya uenyekiti wa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameihimiza serikali ya Burundi kuahirisha chaguzi kwani mazingira hivi sasa hayawezi kuhakikisha uchaguzi huru na haki.

Mwandishi: Amida Issa
Mhariri:Iddi Ssessanga