1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala nchini Nigeria chapoteza wingi wa wabunge

10 Aprili 2011

Chama cha rais Goodluck Jonathan kimepata upinzani mkali katika uchaguzi uliofanyika jana Nigeria. Kulitokea matatizo ya hapa na pale lakini waangalizi wameridhika.

https://p.dw.com/p/10r0Y
Rais wa Nigeria, Goodluck JonathanPicha: AP

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge nchini Nigeria yasiyo rasmi yanaonesha chama tawala cha "Peoples Democratic Party" PDP, kimepoteza udhibiti wa bunge. Chama hicho cha rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, kinatarajiwa kupoteza wingi wa wabunge, kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa chama cha upinzani cha Action Congress of Nigeria, ACN, kusini magharibi mwa nchi. Chama cha PDP vile vile kimepata upinzani mkali kutoka kwa chama cha Congress for Progressive Change, CPC, katika baadhi ya maeneo ya kaskazini.

Magazeti kadhaa yemeripoti kuwa spika wa Bunge, Dimeji Bankole na binti wa rais wa zamani wa nchi hiyo Olusegun Obasanjo wanaelekea kupoteza viti vyao vya ubunge.

Kuna taarifa za masunduku ya kura kuibwa na kutokea mapigano kati ya wafuasi wa vyama vinavyohasimiana katika baadhi ya sehemu za jimbo la Niger Delta. Hata hivyo waangalizi wa uchaguzi huo wanasema kulikuwa na maendeleo makubwa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita. Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika Jumamosi ijayo, na utafuatiwa na uchaguzi wa magavana Aprili 26.