1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za mwishoni mwa wiki hii

Ramadhan Ali11 Oktoba 2007

Kinyan'ganyiro cha kuania nafasi kwa finali za kombe la Ulaya 2008 nchini Austria na Uswisi na kile cha Kombe la Afrika la mataifa nchini Ghana,kinauma Ulaya na Afrika.

https://p.dw.com/p/C7nS

Mwishoni mwa wiki hii,Ligi zinasimama na timu za taifa zinaingia uwanjani ama kukata tiketi zao kwa kombe lijalo la Ulaya 2008 huko Uswisi na Austria au Kombe la Afrika la mataifa nchini Ghana.Kwa mashabiki wa Rugby,mabingwa wa 1995- Afrika kusini, watakuwa uwanjani kesho (jumapili) kuchuana na Argentina katika nusu-finali ya kwanza.Katika ile ya pili,wenyeji Ufaransa, wana miadi na mabingwa wa dunia Uingereza.

Mohammed Abdulrahman, anawafunulia kawa kwa upana zaidi akiwasimulia juu ya changamoto hizo za za leo na kesho:

Tukianza na kanda ya Afrika, mabingwa watetezi-Misri wanateremka leo uwanjani mjini Cairo kupambana na Botswana katika changamoto za kundi la 2.Misri,inataka kurudi Cairo,januari, mwakani na kombe lao kutoka Accra.

Leo pia ni zamu ya Burundi kuingia uwanjani jioni hii mjini Nouakchott.Mauritania watakua nyumbani kuwakaribisha.

Misri inangoza kundi hili huku waburndi wakishika nafasi ya pili,Botswana ya tatu na Mauritania ikiburura mkia.

Katika changamoto hizi,washindi wa kwanza katika kila kundi wantaenda Ghana kwa kombe la Afrika linaloanza Januari 20 hadi februari 10,mwakani.

Katika kanda ya Ulaya,kuania tiketi kwa finali za Euro 2008 huko Uswisi, Ujerumani na Croatia zinaweza leo kutia kikapuni tiketi zao na kuwa timu za kwanza kuwasili finali hizo.

Makundi yote 7 yako uwanjani,lakini wajerumani wanahitaji pointi 1 tu kutoka Ireland, mjini Dublin, ili kuhetimisha safari yao ya Uswisi.Croatia kwa upande wake, inahitaji ushindi dhidi ya Israel na Estonia ili kuepuka shoka la kuwafyeka watakapokutana na waingereza- kuhakikisha nao wanawafuata wajerumani kwa safari ya Uswisi.

Kocha wa ujerumani Joachim Loew ameonya hata hivyo kwamba mpambano huu katika uwanja wa Croke Park utakua mteremko tu kwao.

Croatioa inayoongoza kwa pointi 3 mbele ya Uingereza na yenye mwanya wa pointi 5 mbele ya Russia,haioneshi itapewa taabu na Israel.Uingereza kwa upande wake, itapata mteremko katika bunde la Estonia.

Mabingwa na makamo bingwa wa dunia-Itali na Ufaransa-wote wanacheza nyumbani.Itali ina miadi na Georgia wakati Ufaransa invikaribisha visiwa vya Faroe.Zote mbili-Itali na Ufaransa, hazitakua na shida kutamba.

Mabingwa watetezi Ugiriki, chini ya kocha wao mjerumani Otto Rehagel,wametulia kabisa kileleni mwa kundi C wakiwa na pointi 19 kutoka mapambano 8.Leo wanacheza nyumbani na Bosnia-Herzegovina walio pointi 6 nyuma yao.

Mabingwa wa dunia Itali wakishinda leo,basi tikiti yao ya kwenda Uswisi na Austria,haiku mbali.

Kwa mashabiki wa kombe la dunia la Rugby,leo na kesho –asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano nchini Ufaransa:Wenyeji Ufaransa wanataka kuwatia munda mabingwa watetezi Uingereza hii leo na kuwavua taji na mapema.Waingereza wana ajenda nyengine-kurudi na kombe walikotoka nalo-London.

Kwa mashabiki wa Afrika, macho watayakodoa katika mpambano wa kesho baina ya Afrika Kusini na Argentina.Springboks walitwaa kombe la dunia nyumbani,1995 na baada ya mahasimu wao wakubwa kutolewa nje na mapema-Australia na New Zealand, Springboks wanahisi ni nafasi nyengine ya kurudi Johannesberg na taji la dunia.

Waargentina ambao hawakuwahi kupindukia robo-finali katika kombe hili,wameapa kutorejea Buenos Aires na mapema.Finali jumamosi ya Oktoba 22 ndio shabaha yao.