1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China kuruhusu wanandoa kuwa na watoto watatu

Lilian Mtono
31 Mei 2021

Kamati kuu ya chama cha Kikomunisti cha China imeamua kwenye mkutano uliofanyika Jumatatu hii na kuongozwa na rais Xi Jinping kuruhusu familia kuwa na hadi watoto watatu katika siku za usoni

https://p.dw.com/p/3uFCJ
China Familie
Picha: Xinhua/imago images

Shirika la habari la China, Xinhua limeripoti kwamba wale waliokuwa kwenye mkutano huo waliamua kuanzisha sera na hatua muhimu za kukabiliana na ongezeko la watu wenye umri mkubwa. Ripoti zimesema kwamba hatua ya kuwaruhusu mke na mume kuwa na hadi watoto watatu itakuwa ni ya muhimu na itauboresha mfumo wa idadi ya watu nchini China.

Licha ya China kuondoa sera yake ya mtoto mmoja ya mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kwamba watu hawakuizingatia sana fursa hiyo. Mwaka 2020, kiwango cha uzazi cha China kilishuka hadi karibu asilimia 1.3 kwa mwanamke mmoja, ambacho ni chini ya takriban asilimia 2 kilichotakiwa ili kuendeleza uthabiti katika kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu.

Sera ya mtoto mmoja ilianzishwa mahususi kwa ajili ya kuzuia ongezeko la haraka la idadi ya watu.

BdTD China Peking Kinder mit Masken spielen in Nähe des Eingangs zur Verbotenen Stadt
Watoto wakicheza nje ya lango la mji uliopigwa marufukuPicha: Reuters/T. Peter

Kuanzia mtoto mmoja hadi watatu. Hii itasaidia?

Kulea familia katika majiji ya China inaweza kuwa ni ghali mno kwa wazazi.

Mtaalamu wa sosholojia katika chuo cha Kings cha London Ye Liu, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba "bado kunakosekana mapendekezo thabiti ya kisera katika kushughulikia vizingiti vikubwa vitatu vnavosababisha familia na hasa wanawake kujizuia kuwa na watoto wengi."

Nchini China gharama za malezi ya mtoto, ubaguzi wa ajira dhidi ya kina mama na kukosekana kwa kanuni za kuwezesha malezi ya mtoto kwa pamoja vinaonekana kuwa vizingiti dhidi ya malengo ya serikali ya kuanzisha sera hiyo mpya, alisema.

Kundi la watu wenye uwezo wa kufanya kazi nalo limepungua kwa kiasi kikubwa, hali inayoibua wasiwasi wa kuibuka kwa mzozo unaohusiana na data ya idadi ya watu hivi karibuni. Sensa ya karibuni kabisa iliyochapishwa mwezi uliopita imeonyesha ongezeko la chini mno la idadi ya watu nchini China kuwahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1950. Sensa ya China hufanywa kila baada ya muongo mmoja.

Taifa hilo bado linafikiria kuwa moja ya mataifa yenye idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni kwa takriban watu bilioni 1.4.

DW