1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China, Marekani zaanza mkutano wa kimkakati

Mohammed Khelef6 Juni 2016

Mkutano kati ya Marekani na China unaowajumuisha maafisa wa ngazi za juu wa masuala ya nje na biashara umeanza mjini Beijing ili kuimarisha mafungamano na kupunguza hali ya mivutano kati ya mataifa hayo makubwa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/1J12R
Viongozi wa Marekani na China kwenye siku ya kwanza ya mkutano wa pamoja juu ya biashara na siasa za nje za mataifa yao mjini Beijing, China.
Viongozi wa Marekani na China kwenye siku ya kwanza ya mkutano wa pamoja juu ya biashara na siasa za nje za mataifa yao mjini Beijing, China.Picha: Reuters/S. Loeb

Mkutano huo wa kila mwaka ulifunguliwa na Rais Xi Jinping wa China ukipewa jina la Mdahalo wa Kimkakati na Kiuchumi, huku hata kwenye mwanzo siku yake ya mwanzo hivi leo, tayari hali ya wasiwasi juu ya madai ya China kulitwaa peke yake eneo lote na Bahari ya Kusini ya China ikitawala.

Huku akionekana kuusema msimamo wa Marekani kuelekea mzozo huo kati ya China na majirani zake, Rais Ji aliwaambia wajumbe wa mkutano kwamba nchi yake inachokitaka ni mashirikiano na sio mashindano.

"Eneo hili la Pasifiki linapaswa kuwa jukwaa la mashirikiano ya jumla na sio uwanja wa mashindano. China hutumia diplomasia ya ujirani, heshima na manufaa kwa pande zote husika na inadhamiria kuendeleza amani, utulivu na maendeleo ya eneo la Asia na Pasifiki. Na nchi hizi mbili, China na Marekani, zinaweza kushirikiana kuendeleza uhusiano wa kirafiki unaojumuisha wote na sio unaowatenga wengine."

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, aliitolea wito serikali mjini Beijing kuungana na majirani zake kusaka suluhisho kwa wasiwasi unaongezeka baina ya majeshi ya majini ya Marekani na China. Jeshi la Marekani lipo kwenye eneo hilo kwa kile linachosema ni kuwalinda marafiki zake, Japan na Korea Kusini.

Rais Xi Jinping wa China (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (katikati), katika mkutano wa kimkakati kati ya mataifa yao mjini Beijing.
Rais Xi Jinping wa China (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (katikati), katika mkutano wa kimkakati kati ya mataifa yao mjini Beijing.Picha: Reuters/D. Sagolj

Marekani yataka diplomasia na China

Katika kile kinachoonekana kuwa ni kujibu kauli ya Rais Xi Jinping, juu ya wasiwasi wa uingiliaji kati wa Marekani, alisema nchi yake inahitaji zaidi diplomasia.

"Tunatafuta suluhisho la amani kwa mgogoro huu wa Bahari ya Kusini ya China. Sisi si wadai. Hatuegemei upande wa mdadi yoyote kwenye hili, isipokuwa msimamo wetu pekee ni kuwa tusitatuwe mzozo huu kwa hatua za upande mmoja tu, tuutatuwe kwa kutumia utawala wa sheria, kupitia diplomasia, kupitia mazungumzo, na tunataka mataifa yote kusaka suluhisho la kidiplomosia, linalotokana na viwango vya kimataifa na utawala wa sheria."

Mbali ya madai hayo ya wasiwasi wa majirani wa China kwa kile wanachokiita "ubabe" wa taifa hilo kubwa kiuchumi na kijeshi kwenye eneo zima la Asia ya Kusini, Marekani inaitaka pia nchi hiyo kuharakisha mipango ya kupunguza uwezo wa ziada wa kuzalisha, unaolalamikiwa na washirika wake wa kibiashara kwamba unashusha kwa kasi thamani ya bidhaa kwenye masoko yao, na hivyo kutishia maelfu ya nafasi za ajira.

Itakumbukwa kuwa Marekani imeweka sheria kali za kukabiliana na kugeuzwa kuwa jalala la bidhaa dhaifu kutoka China, huku Umoja wa Ulaya nao ukisema unaangalia uwezekano wa kuchukuwa hatua kama hiyo.

Hata hivyo, pande zote mbili, China na Marekani, zimeitumia siku ya kwanza ya mkutano huu wa kimkakati kuelezea utayari wao wa kuimarisha mahusiano na kurekebisha tafauti zao.

Mataifa hayo ndio wachangiaji wakubwa kabisa kwenye mfuko wa kilimwengu wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, na kuimarika kwa uhusiano wao kibiashara na kiusalama kuna maana kubwa kwa mafanikio ya mfuko huo ulioanzishwa na Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Hamidou, Oummilkheir