1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na India kuboresha ushirikiano

14 Mei 2015

Rais wa China Xi Jinping amesifu uhusiano kati ya nchi yake na India, ambao amesema umeanza kuboreka kati ya nchi hizo kubwa barani Asia. Hayo ameyasema akikutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi nchini China.

https://p.dw.com/p/1FPqj
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi (Kushoto), na mwenyeji wake, Rais wa China, Xi Jinping
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi (Kushoto), na mwenyeji wake, Rais wa China, Xi JinpingPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Viongozi hao wamekutana katika jumba la wageni la kifahari katika mji wa Xian, ambao ni makao makuu ya mkoawa Shaanxi. Rais Xi wa China amesema mahusiano kati ya nchi yake na India yamo katika kipindi cha utengamano, yakiwa na mustakabali wenye matarajio mema.

Mazungumzo kati ya viongozi hao wa mataifa mawili makubwa na yanayoongoza kwa idadi kubwa ya watu, kwa pamoja yakiwa na wakazi bilioni 2.6, yamejikita juu ya mahusiano hayo yanayozidi kushamiri, licha ya ushindani mkubwa kati yao, na mifumo tofauti ya kisiasa.

Viongozi wenye mamlaka makubwa

Kuboreka kwa ushirikiano kati ya China na India kumeshika kasi kwa wakati huu, kutokana na mamlaka binafsi ya viongozi wa sasa wa nchi hizo, ambao wanatajwa kuwa na nguvu sana kuliko watangulizi wao wa miaka ya hivi karibuni.

Viwanda vya China vitanufaishwa na soko la India
Viwanda vya China vitanufaishwa na soko la IndiaPicha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu Modi aliianza ziara yake ya China kwa kuyatembelea makumbusho ya wapiganaji maarufu wa kichina wa Terra Cotta, na hekalu la madhehebu ya Buddha ambayo yanaonyesha ushirikiano wa kijadi baina ya mataifa hayo makubwa katika nyanja ya utamaduni.

Akizungumza nchini China, Waziri Mkuu Narandra Modi amesema huu ni muda wa India na China.

''Karne ya 21 ni karne ya Bara Asia, karne ya kupigania uhuru. China na India zinapaswa kufanya kazi bega kwa bega kuendeleza amani na utengamano duniani, ni jukumu ambalo muda unatutaka tulitimize.'' Amesema waziri mkuu wa India.

Heshima isiyo ya kawaida

Katika ziara yake kwenye makumbusho ya wapiganaji maarufu wa kichina, Waziri Mkuu Modi alisindikizwa na mwenyeji wake, rais Xi Jinping. Si kawaida kwa marais wa China kuambatana na wageni wao katika ziara kama hizo. Xi amekariri kauli ya mgeni wake kuhusu kuimarika kwa ushirikiano kati ya India na China, akisema utaleta tija katika sekta ya maendeleo.

Narendra Modi akitembelea hekalu la wabuddha wakati wa ziara yake China
Narendra Modi akitembelea hekalu la wabuddha wakati wa ziara yake ChinaPicha: UNI

China inaitazama India kama soko kwa bidhaa zake za viwandani, zikiwemo treni za kasi kubwa, na ujenzi wa vinu vya nyuklia. Kwa upande mwingine India inaiona China kama fursa ya uwekezaji kwenye sekta yake changa ya viwanda na ujenzi wa miundombinu.

Narendra Modi anatafuta njia ya kupunguza nakisi ya dola bilioni 48 katika biashara kati ya India na China, kwa kuzitafutia masoko nchini China bidhaa zinazotoka katika viwanda vya India.

Nchi hizo mbili zinatazamiwa kusaini mikataba ya biashara yenye thamani ya dola bilioni kumi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la China Daily, katika toleo lake la leo.

Mbali na biashara, Modi na Xi pia watazungumzia masuala ya kisiasa, zikiwemo njia za kumaliza mvutano katika eneo lao la mpaka, ambalo mwaka 1962 lilizua mzozo uliodumu kwa mwezi mzima. Hakuna suluhisho la haraka linalotarajiwa kupatikana kuhusiana na mvutano huo, ingawa nchi hizo zimekuwa zikifanya mazungumzo ya mara kwa mara kuepusha makabiliano.

Waziri Mkuu wa India pia atafanya mazungumzo na waziri mkuu wa China Li Keqiang kesho Ijumaa, kabla ya kwenda mjini Shanghai katika shughuli zinazohusu ushirikiano wa kibiashara.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri:Josephat Charo