1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Ujerumani kuimarisha uhusiano

30 Machi 2014

Ujerumani na China zimeahidi kuimarisha mkakati wao wa kibiashara wakati wa ziara ya kihistoria ya Rais Xi Jinping wa Chinannchini Ujerumani ambayo imeshuhudia kusainiwa mikataba kadhaa ya kiuchumi Ijumaa.(28.03.2014)

https://p.dw.com/p/1BYSE
Kansela Angela Merkel na Rais Xi Jinping wa China katika mkutano na waandishi wa habari Berlin.(28.03.2014).
Kansela Angela Merkel na Rais Xi Jinping wa China katika mkutano na waandishi wa habari Berlin.(28.03.2014).Picha: Reuters

Kampuni kuu ya kutengeneza magari nchini Ujerumani imechukuwa nadhari kuu katika kituo cha tatu cha ziara ya Xi barani Ulaya ambapo kampuni kuu ya magari ya Daimler ikitangaza kufikiwa kwa mkataba wa kutengeneza magari na wenzao wa China wenye thamani ya euro bilioni moja.

Ushirika huo na Shirika la Magari la China la (BAIC Group) unapanga kuongeza uwezo wa uzalishaji katika mradi wao wa pamoja wa Beijing Benz (BBAC) ifikapo mwaka 2015.

Miongoni mwa mikataba mengine iliosainiwa hapo Ijumaa Benki ya Ujerumani Bundesbank na Benki ya Watu wa China zimekubaliana juu ya nia ya kuanzisha kituo cha fedha kushughulikia malipo ya shughuli za kibiashara kwa kutumia sarafu ya China ya yuan katika mji wa Frankfurt.

Ujerumani ni mshirika mkuu wa biashara wa China katika Umoja wa Ulaya wakati taifa hilo kubwa kabisa la Asia ni soko kuu wa mashine za Ujerumani,teknolojia na magari.

Ukraine yajadiliwa

Viongozi wa nchi hizo mbili wamesema wamejitolea kuimarisha uhusiano wao kwa mashauriano ya kila mara kuhusu masuala ya dunia na kanda na uratibu wa karibu zaidi katika Umoja wa Mataifa,Kundi la Mataifa 20 ya nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi na mashirika mengine ya kimataifa.

Wote wawili Merkel na Xi ambaye ni rais wa kwanza wa China kuitembelea Ujerumani katika kipindi cha miaka minane wamelizungumzia suala la Ukraine.

China ambaye kwa kawaida ni mshirika wa Urusi ilijitowa katika kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya rasimu ya azmio lenye kuilani kura ya maoni inayoungwa mkono na serikali ya Urusi ambayo imepelekea kunyakuliwa kwa jimbo la Crimea na Urusi.Pia imejitowa katika kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Alhamisi ambayo haijifungi kisheria yenye kutangaza kujitenga kwa Crimea sio halali.

Rais Xi Jinping wa China akiwa Düsseldorf (29.03.2014)
Rais Xi Jinping wa China akiwa Düsseldorf (29.03.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Rais Xi amesema China haina maslahi binafsi katika suala la Ukraine na kwamba pande zote zinazohusika zinatakiwa kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kidiplomasia kwa mzozo huo.

Kansela Merkel amesema Ujerumani imekuwa wazi katika suala la kutetea kuheshimiwa kwa mamlaka ya dola na sheria ya kimataifa.

Haki za binaadamu muhimu

Wakati Rais Xi hakugusia masuala ya haki za binaadamu Merkel amesema suala hilo ni sehemu muhimu katika mazungumzo kati ya China na Ujerumani na kusisitiza umuhimu wa uhuru wa kuzungumza katika dunia inayoendelea kubadilika.

Kansela Angela Merkel na Rais Xi Jinping wa China katika mkutano na waandishi wa habari Berlin.(28.03.2014).
Kansela Angela Merkel na Rais Xi Jinping wa China katika mkutano na waandishi wa habari Berlin.(28.03.2014).Picha: Reuters

Ziara ya Xi inakuja kabla ya wiki ya kufunguliwa kwa maonyesho makubwa kabisa kuwahi kufanyika ya msanii mpinzani wa Kichina Ai Wenwei kufunguliwa mjini Berlin.Msanii huyo mwenye kuikosoa serikali hawezi kuhudhuria maonyesho hayo kutokana na kutaifishwa kwa paspoti yake na serikali ya China hapo mwaka 2011 baada ya kuwa kizuizini kwa takriban miezi mitatu.

Akiandamana na mke wake muimbaji Peng Liyuan ,Rais Xi alilakiwa kwa heshima za kijeshi katika viwanja vya Kasri la Rais na mwenyeji wake Rais Joachim Gauck wa Ujerumani mwanaharakati wa haki za binaadamu wa zamani wa Ujerumani Mashariki.Nje ya viwanja hivyo kulikuwa na kama wanaharakati 50 wa Tibet waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili nchini Ujerumani Rais Xi anatembelea makao makuu ya Umoja wa Ulaya yalioko Brussels Ubelgiji.Hii ni ziara ya kwanza ya Xi barani Ulaya tokea awe rais wa China na imejikita zaidi katika uwekezaji wa kigeni ambapo alipokuwa nchini Ufaransa alisaini makubaliano ya kuagizia ndege kutoka kampuni kubwa kabisa ya ndege barani Ulaya ya Airbus yenye thamani ya euro bilioni 10. Ziara yake nchini Brussels pia inaonekana kama ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na umoja huo wenye nchi wanachama 28.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters/dpa

Mhariri : Caro Robi