1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China: Watu zaidi ya 4500 waambukizwa virusi vya Corona

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
28 Januari 2020

Hadi kufikia sasa zaidi ya watu 100 wameshafariki kutokana na homa inayosababishwa na virusi hivyo. Wengi wa watu walioambukizwa wapo katika mji wa Wuhan ambapo ndipo vilipozuka virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3WuSh
China Wuhan Medzinisches Personal in Schutzanzügen
Picha: Getty Images/AFP/H. Retamal

Idadi ya vifo vya kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona imeongezeka hadi kufikia watu 106 hali ambayo inaleta wasiwasi ulimwenguni kote. Kisa cha kwanza kimeripotiwa nchini Ujerumani. Maelfu ya raia wa kigeni wamekwama katika mji huo wa Wuhan, huku mataifa tajiri ikiwa ni pamoja na Marekani na nchi nyengine zinajiandaa kuwaondoa raia wake kutoka kwenye jiji la Wuhan ambalo ndio kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.

Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) Khamis Hassan Bakari mwenye umri wa miaka 39 kutoka Tanzania, alipozungumza na shirika la habari la AFP amesema maisha yamebadilika katika mji wa Wuhan,ameeleza kuwa hofu imetanda kila mahala. Daktari Bakari amesema usafiri umesitishwa, mitaa haina chochote na hata sherehe za sikukuu ya mwaka mpya ni kama hazipo kabisa.

China imeweka marufu ya usafiri kuingia na kutoka mji w a Wuhan
China imeweka marufu ya usafiri kuingia na kutoka mji w a WuhanPicha: Getty Images/AFP/H. Retamal

Bakari amekuwa kiongozi kwa mamia ya mawanafunzi na raia wa Kiafrika ambao hawana matarajio kama wataweza kuondoka kutoka kwenye mji huo. Yeye na kamati ndogo ya madaktari wenzake kutoka Afrika Mashariki mara kwa mara wanatuma taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mlipuko wa virusi vya corona na yanayoendelea. taarifa hizo zinafikishwa kwa wanafunzi zaidi ya 400 wa Kitanzania walio katika jiji la Wuhan vile vile kwa mamia ya wananchi wa Tanzania walio mahali pengine nchini China. Taarifa hizo kwa kiasi kikubwa huwa katika lugha ya Kiswahili. Kikundi hicho kinalenga kuwahamasisha Waafrika juu ya umuhimu wa kuchukua hatua za tahadhari.

Wanafunzi wa Tanzania wameutaka ubalozi wa nchi yao kuwafahamisha kuhusu juhudi za serikali juu ya kuwaondoa kutoka kwenye mji wa Wuhan ambapo wamesema ubalozi umewaambia kuwa mamlaka zinalifanyia kazi suala hilo.

Daktari Bakari amefahamisha kwamba kamati yake imeanza kukusanya simu za wawakilishi wa wanafunzi wa vyuo vikuu vyote katika mji wa Wuhan kwa ajili ya kupokea ripoti juu ya matatatizo yoyote au pia kufahamishana namna ya kuweza kusaidiana.

Hali hiyo ya wasiwasi anaielezea pia mwanafunzi mmoja wa Ethiopia wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha mjini Wuhan, ambaye anasema anajihisi kama mfungwa na kwamba huenda hali hiyo ikasababisha mamlaka ya China kukatiza ufadhili wa masomo yao.

Vyanzo:/AP/DPA