1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaitaka Uingereza kukoma kuingilia suala la Hong Kong

Angela Mdungu
4 Julai 2019

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza Jeremy Hunt, ameahidi kuendelea kuishinikiza  China kuhusu njia za  nguvu inazotumia dhidi ya waandamanaji mjini Hong Kong huku mzozo wa kidplomasia ukiongezeka.

https://p.dw.com/p/3LZBo
Hongkong Regierungschefin Carrie Lam
Picha: picture-alliance/AP Photo/Vincent Yu

Hunt amerejelea kuwa kutakuwa na athari iwapo China itakiuka makubaliano yalioafikwa kuhusu haki mjini Hong Kong wakati Uingereza ilipoikabidhi uthibiti.

Akizungumza na BBC radio , Hunt alikataa kutaja hatua maalum zitakazochukuliwa lakini akasema kuwa hatua hizo zinapaswa kuachwa wazi   na kwamba kile alichotaka kufanya ni kuweka ujumbe wazi kuwa hili sio jambo ambalo litapuuzwa na kuendelea mbele  lakini litakuwa suala muhimu sana kwa Uingereza.

Baada ya onyo la kwanza la Hunt siku ya jumanne la kuchukuwa hatua dhidi ya China , wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya China imejibu kwa kumshtumu Hunt kwa kujiingiza katika nadharia za kikoloni.

Balozi wa China nchini  Uingereza Liu Xiaoming hapo jana alizungumza na waandishi habari  na kuitaka Uingereza kukoma kuingilia masuala ya ndani ya Hong Kong.

Balozi huyo pia ameonya kuwa hatua hiyo inatishia kuendelea kuharibu uhusiano kati ya mataifa hayo mawili .

Liu Xiaoming baadaye alitakiwa kufika katika wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Uingereza mjini London .

Hunt atetea muingilio wa Uingereza katika suala la HongKong

England Außenminister Jeremy Hunt
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza- Jeremy HuntPicha: picture-alliance/NurPhoto/W. Szymanowicz

Hii leo Hunt amerejelea kuwa hawaungi mkono waandamanaji wanaozua rabsha waliovamia bunge la Hong Kong lakini amesema kuwa hawapaswi kuandamwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Vyombo vya habari na hasa  vya serikali ya China vinailaumu Uingereza Mareknai na nchi nyingine za Magharibi kwa kuwapa kiburi na nguvu waandamanaji.

Mamia ya waandamanaji waliingilia bunge la Hong Kong siku ya Jumatatu baada ya maandamano ya kuadhimisha siku ya kurejeshwa kwa uongozi wa China mwaka 1997 chini ya muundo wa serikali moja  na mifumo miwili inayojumuisha uhuru ambao haupatikani katika China bara ikiwa ni pamoja na uhuru wa kufanya maandamano.

Hii inafuatia wiki za maandamano dhidi ya msuada ulioahirishwa wa kuwahamisha washtakiwa kutoka Hong Kong hadi katika mahakama za China bara zinazothibitiwa na chama cha kikomunisti.

Hunt ameongeza kuwa, wanaiona hali hiyo kuwa ya kutatanisha  na kile wanachokihitaji ni kwa Hong Kong kurejelea mkataba ulioko kati ya Uingereza na China kutoka mwaka 1984 na kuutekeleza.