1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaituhumu Taiwan kwa kutambua uhuru wa Kosovo

P.Martin20 Februari 2008

Kosovo iliyojitangazia uhuru wake kutoka Serbia,ipo mbali na China,lakini athari za hatua hiyo ni kubwa mno kwa taifa kubwa la China.

https://p.dw.com/p/DAcF

Suala la Kosovo linagusia kiini cha mfumo wa kikatiba wa taifa jipya la China.Mfumo huo umefanana na ule wa shirikisho la jamhuri za zamani za Soviet Union na Yugoslavia.Baada ya Kosovo kujitangazia uhuru wake kutoka Serbia,kumezuka hatari ya kuanzishwa mfano usiowahi kutokea hapo awali,miongoni mwa makundi 56 ya makabila madogo yanayotambuliwa nchini China.Zaidi ya nusu ya ardhi ya China inakaliwa na makundi hayo ya kikabila.Si hilo tu bali kuna maeneo mengine yenye uongozi maalum kama vile Hong Kong na Macao pamoja na eneo la Taiwan.Uhusiano wa maeneo hayo pamoja na Beijing ni kama ule wa Kosovo na Belgrade.

Lakini kinachofadhaisha zaidi ni ukweli kuwa tangazo la Kosovo limeungwa mkono na Marekani na madola makuu ya Ulaya.Msimamo thabiti wa nchi za magharibi kutambua haki za wachache kujitawala wenyewe na kujitoa kwenye mamlaka ya Serbia umeichochea Beijing kueleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu yale yanayotokea Kosovo.Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China,Liu Jianchao ameonya kuwa hatua iliyochukuliwa Kosovo huenda ikavuruga kanda nzima ya Balkan.Kinachohofiwa na China ni kuwa hatua iliyochukuliwa na madola makuu ya Ulaya na Marekani kuitambua Kosovo moja kwa moja huenda ikayafanya makabila madogo ya Kichina kama vile Watibet au Wauighur wa Wilaya ya Xinjiang kupigania kupewa mamlaka zaidi ya kujitawala.

Maudhi zaidi kwa China ni kuwa tangazo la uhuru wa Kosovo limetolewa wakati ambapo Taiwan katika muda wa mwezi mmoja ujao itaitisha kura ya maoni yenye mabishano,iwapo kisiwa hicho kinachojitawala kipeleke maombi ya kujiunga katika Umoja wa Mataifa kwa jina la Taiwan badala ya jina lake rasmi Jamhuri ya China.

China na Taiwan zilitengana mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1949.Bara China,inashikilia kuwa pande hizo mbili hatimae zitaungana na zitakuwa chini ya udhibiti wa Beijing,ikilazimika hata kwa nguvu.

Taiwan ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kuipongeza Kosovo kwa kujitangazia uhuru wake.Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Taiwan ilisema kuwa Taiwan ni miongoni mwa jumuiya ya kimataifa inayoheshimu demokrasia na uhuru na serikali ya Taiwan imefurahi kuona Wakosovo wakivuna matunda ya uhuru na demokrasia.China wala haijakawia kuituhumu Taiwan kwa kuthubutu kutamka hayo na kusema kuwa Taiwan kama sehemu ya China haina haki yo yote ile kuchukua hatua ya kama hiyo.

Lakini China imesema kuwa itapeleka Kosovo tume ya maafisa wa polisi 17 kusaidia kulinda amani.China tangu mwaka 2004 imekuwa ikishiriki katika tume ya Umoja wa Mataifa kusimamia amani huko Kosovo.