1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yakumbuka mauaji ya Tiananmen

4 Juni 2014

China imeweka ulinzi mkali katikati ya mji mkuu Beijing, katika kumbukumbu ya miaka 25 ya ukandamizaji uliofanywa na serikali kuyazima maandamano ya kutaka demokrasia yaliyofanyika katika uwanja wa Tiananmen.

https://p.dw.com/p/1CBfM
China Peking Platz des himmlischen Friedens 03.06.2014
Picha: Getty Images

Tukio hilo la kistoria lililosababisha umwagaji damu limesalia kuwa mada isiyozungumziwa hadharani katika nchi hiyo ya Kikomunisti. Katika mkesha wa kumbukumbu ya miaka 25 ya ukandamizaji wa serikali ya China dhidi ya maandamano yaliyofanyika katika uwanja wa Tiananmen, Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa zimeitaka serikali ya China kuwaachilia huru watu waliokamatwa katika siku za karibuni, wakati mji wa Hong Kong ukijiandaa kwa maombi ya kila mwaka ya kuwasha mishumaa ambayo watu watu laki mbili wanatarajiwa kuhudhuria mwaka huu.

Maelfu ya polisi na wanajeshi, wengine wao wakiwa na bunduki za rashasha wamewekwa katika mji mkuu Beijing. Malori ya polisii yamejaa karibu na ndani ya uwanja wa kihistoria wa Tiananmen. Ulinzi pia umeimarishwa hasa kufuatia wimbi la mashambulizi ya karibuni ambayo serikali inawalaumu wanaharakati wanaopigania kujitenga katika eneo la magharibi la Xinjiang.

Watalii na wachuuzi wanakaguliwa

Watalii na wachuuzi wanaendelea na shughuli zao katika uwanja huo wa umma katikati ya Beijing, lakini polisi waliovalia sare na wengine waliovalia nguo za kiraia wamewekwa katika kila eneo na wanakagua vitambulisho vya wapita njia.

Peking Platz des himmlischen Friedens 04.06.2014
Wanejeshi wakiweka doria katika mji mkuu BeijingPicha: Reuters

Mamia ya raia ambao hawakuwa na silaha -- kwa mujibu wa takwimu nyingine, zaidi ya 1,000 – waliuawa kwenye msako wa Juni 3 hadi 4 mwaka wa 1989, wakati wanajeshi walipoyavunja maandamano yaliyokuwa yamedumu miezi kadhaa ya wanafunzi waliokuwa wakidai mabadiliko ya kisiasa. Chen Guang ni mmoja wa wanajeshi waliokuwa katika operesheni hiyo na anasema tukio hilo halijawahi kuondoka akilini mwake "Mimi nilikuwa na hofu. Leo hii najua kuwa wanafunzi hao waliluwa dhaifu na nimekuwa nikijiuliza daima: walikuwa wapi hao waasi waliokuwa wanazungumziwa? Wale wanaoitwa wahalifu? Sikuona hata mmoja wakati huo na hadi sasa sijawaona. "

China yazima kumbukumbu

Tangu wakati huo, China imefanya juu chini kuzima kumbukumbu za wananchi kuhusu ukandamizaji huo, kwa kuzuia kwa kila njia kutajwa tukio hilo katika mitandao ya kijamii na kuwaweka kizuizini wanaharakati, mawakili, wasanii na waandishi wa habari katika wiki za hivi karibuni. hata hivyo Guang anasema tukio hilo haliwezi kusahahulika. "ni miaka 25 sasa. kilichofanyika wakati huo, hakinihusu tu mimi pekee pamoja na kizazi changu, bali kinaathiri kila mtu.

Katika mkesha wa kumbukumbu hiyo, Marekani imesisitiza wito wake kwa China kufanya mageuzi mapana ya kisiasa na kuitaka iwaachilie huru waliokamatwa. Vyombo vya habari vya kigeni mjini Beijing vimeonywa na polisi na wizara ya mambo ya kigeni ya china dhidi ya kukusanya habari zozote zinazohusiana na kumbukumbu hiyo, au vikabiliwe na “mamdhara makubwa”, ikiwa ni pamoja na kupokonywa vibali vyao vya kuwa nchini humo.

Bildergalerie Tiananmen
Picha hii maarufu inayomwonyesha raia aliyejaribu kuuzuia msafara wa vifaru ilienea sana kote dunianiPicha: Jeff Widener/AP

Katika tukio moja lililoripotiwa Jumatatu na Chama cha Waandishi wa Habari wa Kigeni nchini China, kikosi cha waandishi wa habari wa kituo kimoja cha televisheni ya Ufaransa kilizuiliwa na polisi kwa muda wa saa sita wakati wakijaribu kumhoji mpita njia kwenye mitaa ya Beijing.

Tukio hilo lililaaniwa kote lakini miaka 25 baadaye, mamlaka ya chama tawala cha Kikomunisti bado yako imara na mshikamano wake wa kimataifa unaendelea kuongezeka pamoja na ukuwaji wa kasi wa nchi hiyo, ambao umeiweka China katika nafasi ya pili katika orodha ya nchi kubwa ta kiuchumi duniani nyuma ya Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Ssessnga Iddi