1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yawawekea vikwazo maafisa wa Marekani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
10 Agosti 2020

China imetangaza vikwazo dhidi ya wanasiasa 11 wa Marekani pamoja na wakuu wa mashirika yanayongoza harakati za kidemokrasia. Hatua hii ya China ni majibu kwa Marekani baada ya rais Trump kuiwekea vikwazo Hong Kong.

https://p.dw.com/p/3gkaC
China Peking Neuer Außenministeriumssprecher Zhao Lijian
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Wong

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Zhao Lijian alitangaza hatua hiyo leo kwenye mkutano na waandishi wa habari. Amesema leo kwamba Wamarekani hao 11 walivuka mipaka kwenye maswala yanayohusu Hong Kong. Amesema Matendo ya wahusika wa Marekani ni wazi yanaingilia katika mambo ya Hong Kong, yanaingilia kati mambo ya ndani ya China, vitendo hivyo vinavunja sheria za kimataifa na kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa na kwamba China inapinga kabisa na inalaani vikali hatua hiyo.

Mingoni mwa maseneta waliowekewa vikwazo hivyo na China ni pamoja Marco Rubio na Ted Cruz. Maseneta hao wa Marekani wamekuwa wakosoaji wakubwa wa sheria mpya ya usalama wa taifa ambayo China iliweka mjini Hong Kong mwishoni mwa mwezi Juni. Idadi ya Wamarekani waliotajwa na wizara ya mambo ya nje ya China ni sawa na idadi ya maafisa wa Hong Kong na China bara waliowekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani.

Mmiliki wa vyombo vya habari Jimmy Lai aliyekamatwa mjini Hong Kon
Mmiliki wa vyombo vya habari Jimmy Lai aliyekamatwa mjini Hong KongPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Yu

Hatua ya China ya kuwawekea vikwazo raia 11 wa Marekani ni ya hivi karibuni katika malumbano kati ya China na Marekani huku nchi hizo zikitoleana tuhuma za ukiukaji wa haki za kimataifa na kuingiliana kwenye masuala ya ndani. Marekani mnamo siku ya Ijumaa (Agosti 7) ilitangaza vikwazo dhidi ya kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam pamoja na wakuu wa polisi wa sasa na wa zamani, katika agizo lililotiwa saini na Rais Donald Trump. Vikwazo hivyo vinahusu kuzuia mali zozote zinazomilikiwa na walengwa zilizopo nchini Marekani na pia vinawazuia raia wa Marekani kufanya biashara nao.

Wakati huo huo mamlaka ya China imeongeza utekelezaji wake wa sheria mpya ya usalama wa taifa leo Jumatatu, kwa kumkamata mmiliki wa vyombo vya habari Jimmy Lai na kuyavamia makao makuu ya uchapishaji wa magazeti yake. China imesema inaunga mkono kukamatwa kwa mmiliki huyo wa vyombo vya habari Jimmy Lai na polisi wa Hong Kong na imesisitiza juu ya kuwaadhibu vikali wale wote ambao wanashirikiana na makundi kutoka nje katika kuhatarisha usalama wa taifa. Lai, mwenye umri wa miaka 71, amekuwa mmoja wa watetezi maarufu wa harakati za demokrasia katika mji wa Hong Kong na mkosoaji mkubwa wa serikali ya China.

Vyanzo:/ RTRE/AFP/AP/DPA