1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mourinho aendelea kujikuta taabani

27 Oktoba 2015

Jose Mourinho amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na Shirikisho la Soka la Uingereza – FA kutokana na lugha aliyoitumia na vitendo vyake wakati wa mchuano wa mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya West Ham United

https://p.dw.com/p/1Guhv
UEFA Champions League Chelsea vs. Schalke 04
Picha: Reuters/Eddie Keogh

Mourinho alifukuzwa katika eneo la benchi la kiufundi uwanjani baada ya kumtolea maneno makali refarii Jonathan Moss wakati wa kipindi cha mapumziko katika mpambano wa siku ya Jumamosi.

Vilabu vyote viwili, Chelsea na West Ham pia vimeshtakiwa kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wao na vimepewa muda wa hadi Oktoba 29 kujibu mashtaka hayo.

Chelsea tayari wanakabiliwa na faini ya pauni 25,000 baada ya wachezaji wake zaidi ya watano kupewa kadi za manjano wakati wa mechi hiyo ya Ligi ya Premier.

Kando na kadi mbili za manjano alizoonyeshwa Nemanja Matic ( na hivyo kutolewa nje ya uwanja kwa kula nyekundu), Chelsea pia walishuhudia wachezaji wao Cesar Azpilicueta, Willian, Cesc Fabregas, John Mikel Obi na Diego Costa wakirambishwa kadi za manjano uwanjani Upton Park.

Msaidizi wa Mourinho Silvino Louro pia alifukuzwa kwenye benchi la kiufundi wakati wa mechi hiyo na vile vile ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu.

Klabu hiyo pia itatakiwa kueleza wasimamizi wa Ligi ya Premier ni kwa nini Mourinho alikosa kuzungumza na wanahabari baada ya mechi hiyo.

Mechi hiyo ilikuwa ya tano kwa Chelsea kushindwa katika mechi 10 za ligi msimu huu na inawaacha mabingwa hao watetezi wakiwa nambari 15 na alama 11, alama 11 nyuma ya viongozi Manchester City.

Sasa kuna uvumi kuwa chuma cha Mourinho ki motoni, na kuwa anaweza kutimuliwa uwanjani Stamford Bridge wakati wowote, licha ya klabu hiyo kutangaza hadharani mwezi uliopita kuwa bado inamuunga mkono meneja huyo

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Daniel Gakuba