1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Coe anatafuta nafasi ya kuongoza IAAF

7 Agosti 2015

Mmoja wa watu wanaotafuta ruhusa kuanzisha enzi mpya katika mchezo wa riadha Sebastian Coe, amezuru Costa Rica kama sehemu ya kampeni yake ya kutaka wadhifa wa uongozi

https://p.dw.com/p/1GBlB
Großbritannien Sebastian Coe Politiker
Picha: Reuters/Action Images/M. Childs Livepic

Coe amepuuza madai ya kukithiri matukio ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni miongoni mwa wanariadha. Ametoa wito wa kuundwa Tume ya Maadili ili kudhibiti matumizi ya dawa hizo.

Mapema mwezi huu, matokeo yaliyofichuliwa kutoka kwa vipimo 12,000 vya damu iliyotolewa kwa washindani 5,000 yalidaiwa kudhihirisha matukio ya udanganyifu, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari kuhusu data hizo iliyoripotiwa kutengenezwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa – IAAF.

Uchunguzi wa Televisheni ya Taifa ya Ujerumani ARD pamoja na gazeti la Uingereza la Sunday Times uliofanywa kwa ushirikiano na watalaamu ulibaini kuwa mchezo wa riadha umejaa matukio ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku. "Nimeshiriki katika mchezo huu kwa miaka 45, nafahamu kuwa wanariadha wengi nilioshindana nao kutoka klabu yangu hadi katika uwanja wa Olimpiki, watu wengi niliofanya kazi nao katika mchezo wangu wana maoni sawa. Na lazima tutumie kila mbinu ya teknolojia iliyoko kwa sababu changamoto ni kulinda haki za wanariadha wasafi kushindana wakifahamu kuwa wanashindana kwa njia ya usawa. Kwamba kila mwanariadha anashindana akiwa na fursa sawa akifahamu anaweza kushinda au kushindwa".

Sergej Bubka Flash-Galerie
Sergey Bubka mgombea wa urais wa IAAFPicha: DW

Mwanaolimpiki huyo wa zamani wa Uingereza atapambana na bingwa mwenzake wa Olimpiki Segey Bubka katika kinyang'anyiro cha urais wa IAAF mwezi huu wa Agosti. Akizungumza nchini Costa Rica, Bubka ametoa wito wa ushirikiano mpana wa serikali na IAAF ili kupambana na uovu huo. "tunahitaji ushirikiano na msaada imara kutoka kwa upande wa serikali, kwa sababu serikali zina raslimali, zina taasisi na wataalamu wa matibabu na utafiti. Kwa hilo, suala kuu ni kuwa tunahitaji kuendelea kuwekeza pamoja na serikali. Lazima tuziunganishe jamii za michezo na mashirikisho ya kitaifa, kamati ya Kitaifa ya Olimpiki, mashirika ya kupambana na dawa za kuongeza nguvu. Hivi ni vita vikali".

Wagombea hao wawili wana mitazamo tofauti kuhusiana na namna ya kupambana na madai ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Sessanga