1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia na FARC kusaini makubaliano mapya ya amani

Daniel Gakuba
23 Novemba 2016

Serikali ya Colombia na kundi la waasi la FARC watasaini makubaliano mapya ya amani Alhamis, baada ya makubaliano ya kwanza kukataliwa na wananchi katika kura ya maoni iliyopigwa mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

https://p.dw.com/p/2T6FJ
Kolumbien Treffen Regierung und FARC in Bogotá
Wajumbe wa serikali ya Colombia na wa FARC kwenye meza ya mazungumzoPicha: picture-alliance/dpa/EPA/O. Nieto

Pande mbili katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia ambavyo vilidumu kwa takribani miongo mitano, zimethibitisha kuwa makubaliano mapya ya amani yaliafikiwa tarehe 12 mwezi huu wa Novemba. Kwa hali iliyowashtua wengi, makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa awali yalikataliwa katika kura ya maoni, huku baadhi ya watu wakisema yaliwahurumia mno waasi wa FARC.

Tangazo la pamoja la serikali ya Colombia na waasi wa FARC, limesema pande hizo zimekubali kutia saini makubaliano hayo kukomesha uhasama wa muda mrefu ambao umeangamiza maisha ya watu wapatao 220,000.

Wiki iliyopita serikali ya Colombia iliyachapisha nakala ya makubaliano yaliyofanyiwa marekebisho, katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono wa umma.

Upinzani bado haujaridhika

Kolumbien Referendum Gegener des Friedensbakommens scheinen vorne zu liegen Alvaro Uribe
Kiongozi wa upinzani Colombia, Alvaro UribePicha: Reuters/J. Vizcaino

Licha ya juhudi hizo lakini, mpinzani mkuu wa serikali Alvaro Uribe ameyakataa hata makubaliano hayo mapya, akishikilia kwamba mwafaka wowote lazime uidhinishwe kupitia kura ya maoni.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amesema inasikitisha kuona wale aliowaita ''wenye misimamo mikali'' wakiendelea kuyapinga makubaliano mapya licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa kuyafanyia marekebisho ya kina. Rais Dos Santos amekataa hoja za kura mpya ya maoni.

''Alhamis, tutayatia saini makubaliano haya mapya, hapa hapa mjini Bogota. Yatakapokwishasainiwa, yatahitaji bado kukubaliwa na kutekelezwa. Kuhusu utekelezaji, hilo ni jukumu la bunge. Hapo ndipo sheria zote za nchi zinapopaswa kujadiliwa na kupitishwa''. Amesema Santos.

Serikali ya Rais Juan Manuel Santos inatarajiwa kuuwasilisha mswada wa makubaliano hayo bungeni hii leo, ili ukajadiliwe kiundani.

Usitishwaji tete wa mapigano

Kolumbien Juan Manuel Santos Präsident Friedensnobelpreisträger 2016
Rais wa Colombia Juan Manuel SantosPicha: picture-alliance/dpa/M. Duenas Castaneda

Usitishwaji wa mapigano kati ya jeshi la serikali na  waasi umekuwa ukiheshimiwa tangu mwezi Agosti, lakini pande hizo zimesema hali bado ni tete.

''Ni lazima tuingie katika hatua inayofuata ya kuwakusanya wapiganbaji wa FARC na kuwarejesha katika maisha ya kirai, ili kuumaliza mkwamo huu'', amesema rais Santos. Kwa upande wa FARC, makubaliano yatasainiwa na kiongozi wa kundi hiloRodrigo Londono.

Kiongozi wa upinzani, Alvaro Uribe alikuwa amejitolea kukutana kwa mazungumzo na kundi la FARC, lakini kundi hilo limekataa wazo lake, likimtaja kuwa kipingamizi katika mchakato wa kusaka amani.

Katika ujumbe uliotolewa kupitia mtandao wa Twitter, mmoja wa makamanda wa FARC Pablo Catatumbo amesema utawala wa miaka minane wa Uribe ''uligubikwa na ufisadi na umwagaji wa damu'', na kuongeza kuwa azma pekee ya mwanasiasa huyo ilikuwa kulishinda kikamilifu kundi hilo la waasi, azma ambayo hakuweza kuifikia.

Rais Santos amesema inawezekana makubaliano mapya hayatamridhisha kila mtu, akitoa hoja kuwa hilo ni jambo la kawaida kwa makubaliano yoyote. ''Hali hiyo inaeleweka, na inakubalika'', ameongeza rais huyo, na kuonya kuwa kura nyingine ya maoni inaweza kuigawa nchi na kuhatarisha usitishwaji wa mapigano.

Mwandishi: Gakuba, Daniel/rtre, afpe

Mhariri: Hamidou, Oummilkheir