1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP15: Je, bioanuwai ni nini hasa?

Iddi Ssessanga
7 Desemba 2022

Mkutano wa bioanuwai wa Umoja wa Mataifa umeanza huko Montreal, Canada. Mkutano huo wa wiki mbili utajikita katika kuokoa viumbe hai. Lakini Bioanuwai ni nini hasa na kwanini ni muhimu katika maisha yetu?

https://p.dw.com/p/4Kcle
UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Tadodaho Sid Hill, Onondaga Nation
Picha: Christina Muschi/REUTERS

Bioanuwai inamaanisha anuwai jumla ya kibayolojia na kijeni ya viumbe hai na mifumo ya ikolojia kwenye sayari yetu. Viumbe hai vinajumlisha mamalia na mimea na pia kuvu na vijidudu wadogo wanaopatikana kwenye udongo. Mifumo mbalimbali ya ikolojia ni tofauti kama vile Antarctic, misitu ya mvua ya kitropiki, Sahara, misitu ya mikoko, pori la beech nyekundu wa Ulaya ya Kati au maeneo mbalimbali ya baharini na pwani duniani kote.

Soma pia: Mkutano wa Bayoanuwai COP15 wafunguliwa Canada

Makazi hayo yanatupatia sisi wanadamu idadi kubwa ya vitu tunavyohitaji kuishi, kama vile maji, chakula, hewa safi au dawa. Mifumo ya ikolojia hivyo hutoa kile kinachoitwa huduma za mfumo wa ikolojia - na hizi pia zinategemea mwingiliano wa spishi anuwai. Ikiwa sehemu moja moja zitaanguka, kwa mfano kwa sababu spishi zitatoweka, katika hali mbaya zaidi huduma hizi zinazotolewa na asili kwa ajili yetu pia hupotea.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Themenbild
Picha: Christina Muschi/REUTERS

Kwa maneno mengine: Bila mwani au miti hakuna oksijeni. Bila wadudu wa kuchavusha mimea, tusingeweza kuvuna chochote. Kwa sababu zaidi ya theluthi mbili ya mazao yote, ikiwemo aina nyingi za matunda na mboga, kahawa na kakao, hutegemea uchavushaji wa asili kama vile wadudu. Lakini theluthi moja ya spishi zote za wadudu ulimwenguni tayari ziko kwenye hatari ya kutoweka.

Soma: Mazungumzo ya kupambana na upotezaji wa bioanuwai yaanza China

Jinsi maisha yetu yanavyotegemea huduma za asili

Ingawa hatuwezi kuishi bila huduma hizi zinazotolewa na maumbile ya asili, mara nyingi tunazichukulia kawaida, anasema Dave Hole. Mtaalamu huyo wa jenetiki ya ikolojia ameandika utafiti mpya pamoja na wengine kwa shirika la mazingira la Conservation International, ambalo linaangazia huduma za mfumo wa ikolojia.

Kulingana na utafiti huo, hadi asilimia 70 ya mavuno ya dunia yanategemea moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja kuta za vizuwizi na miti shamba, miongoni mwa mambo mengine kwa sababu hulinda maeneo ya kulima mazao ya chakula kutokana na mafuriko. "Tunapokula bakuli la muesli asubuhi, kwa ujumla hatufikirii sana juu ya kile asili imefanya ili kutuwezesha kula muesli hii," Hole alisema katika mahojiano ya DW.

Soma pia:Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa kwanza kuhusu mzozo wa Bioanuwai 

Kamati ya kiserikali ya Umoja wa Mataifa kuhusu Anuwai za Kibayolojia (IPBES) inakadiria kuwa kuna angalau spishi milioni 8, lakini kufikia 2030 hadi milioni moja zinaweza kutoweka milele. Tayari, upotevu wa bayoanuwai umefikia kiwango kikubwa zaidi - sawa na spishi moja inayokufa kila dakika kumi. Kulingana na sayansi, tuko katikati ya kutoweka kwa spishi kwa sita ulimwenguni.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Indigene Protestierende
Waandamanaji wa jamii za asili wakivuruga hotuba ya waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutono wa bioanuwai wa COP15 mjini Montreal, Canada, Desemba 6, 2022.Picha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

Nchini Ujerumani pekee, idadi ya wadudu wanaoruka ilipungua kwa robo tatu kati ya 2008 na 2017. Idadi ya wanyama pori ilipungua kwa asilimia 82 duniani kote, kulingana na IPBES. Idadi ya wanyama na aina za mimea wanaoishi katika maji yasiyo na chumvi imepungua duniani kote kwa asilimia 83 katika miaka 50 iliyopita, na katika Amerika ya Kati na Kusini ilikuwa asilimia 94 ya viumbe hao, kulingana na utafiti wa shirika la mazingira WWF.

Na kulingana na Hole, upotezaji wa anuwai ya kibayolojia hufanyika kwa kasi kubwa - kasi inaongezeka hata.

Wanadamu wanahusika na kutoweka kwa viumbe

Sayansi inakubali: kwa sababu ya kilimo, ufunikaji wa ardhi, usafishaji misitu, uvuvi wa kupita kiasi, kuenea kwa viumbe vamizi na wanadamu, kiwango cha kutoweka leo ni hadi mara 100 zaidi kuliko inavyokuwa pasina ushawishi wa binadamu. 

Elizabeth Maruma Mrema, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Anuwai ya Bayolojia (CBD), ameweka wazi kabisa katika mazungumzo na DW, akisema shughuli za binadamu zimesababisha uharibifu wa asilimia 97 ya viumbe hai duniani.

Takwimu zilizoorodheshwa na mkuu wa CBD ni za kutisha. Kulingana na takwimu hizo, asilimia 75 ya eneo la ardhi kwa sasa limeharibiwa na asilimia 66 ya bahari, asilimia 58 ya nyanda zote za ardhi yowevu zinatishiwa au tayari zimetoweka na nusu ya miamba ya matumbawe tayari imekufa. Mrema anasisitiza kuwa takwimu hizo hazizingatii hata uchafuzi wa sayari kwa taka za plastiki.

UN-Artenschutzkonferenz COP 15 in Montreal, Kanada 2022 | Antonio Guterres, UN-Generalsekretär
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akiondoka baada ya kushiriki mkutano wa kilele wa vijana wa COP15, Desemba 6, 2022.Picha: Andrej Ivanov/AFP/Getty Images

Upotevu wa viumbe hai unatishia sayari na ubinadamu

"Upotevu unaoendelea wa mtaji wetu wa asili unaleta tishio kubwa zaidi kwa wanadamu wote," anaonya Klement Tockner, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Senckenberg ya Ujerumani na Profesa wa Sayansi ya Mfumo wa Ikolojia. "Kwa sababu inapopotea, imepotea milele."

Soma pia: WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani

Pale spishi zinapotoweka kwenye mfumo wa ikolojia, hauporomoki kabisa, lakini unabadilika. "Kadiri tunavyopunguza spishi, ndivyo mfumo unavyoathiriwa zaidi," anaelezea Andrea Perino kutoka Kituo cha Utafiti wa Bioanuwai cha Ujerumani (iDiv) katika Chuo Kikuu cha Halle-Jena-Leipzig.

Kama ilivyo kwa hali ya hewa, pia kuna kile kinachoitwa vidokezo katika mifumo ya ikolojia ambapo matukio yanaweza kutokea na kusababisha hatua zisizoweza kuzuilika, anasema Dave Hole. Mfano wa hii ni msitu wa mvua katika eneo la Amazon. Baada ya msitu huo kufyekwa sana, sehemu iliyobaki pia inazidi kuwa mbaya na mbaya zaidi. Na hiyo inaongeza hatari kwamba msitu wote wa mvua utakufa.

Elizabeth Maruma Mrema
Elizabeth Maruma Mrema, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa UN kuhusu uanuwai wa bayolojia, akizungumza katika mkutano wa habari wa ufunguzi wa COP15 mjini Montreal, Canada, Desemba 6, 2022.Picha: Graham Hughes/AP/picture alliance

Misitu ya kitropiki kama Amazon ni makazi ya karibu theluthi mbili ya viumbe vyote vinavyojulikana duniani kote, na ni muhimu sana kwa tabianchi ya dunia.

Tunahitaji kuilinda vyema asili - kwa maslahi yetu wenyewe

Bila hatua kubwa za kuzuia kupotea kwa bayoanuwai, msingi wa asili wa maisha ya binadamu utapotea kwa kasi isiyokuwa ya kawaida - na madhara ya muda mrefu kwa karibu nyanja zote za maisha.

Asilimia 50 ya uzalishaji wa uchumi wa dunia unategemea moja kwa moja asili, anasema Katibu Mtendaji wa CBD Mrema. "Tunaharibu asili ingawa mapato yetu, chakula chetu, afya zetu na hewa tunayovuta vinaitegemea."

Maajabu ya mnyama Tembo.

Mwandishi: Jeannette Cwienk