1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Ufaransa, Ujerumani zaomba hatua zaidi

Bruce Amani
15 Novemba 2017

Viongozi wa dunia walikuwa mjini Bonn kuyapiga jeki mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi  ambayo yalionekana kugubikwa na hatua ya Rais Donald Trump kutangaza kuwa anaiondoa Marekani katika makubaliano ya Paris 

https://p.dw.com/p/2nheV
UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Espinosa & Macron Bainimarama & Merkel & Guterres
Picha: Reuters/W. Rattay

Akiwahutubia wajumbe 200 mjini Bonn, Kansela Angela Merkel amesema suala hilo litakuwa muhimu katika mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya Ujerumani, lakini hakusema kama anaunga mkono kuwekwa tarehe yoyote ya muda wa mwisho wa kuwachana na matumizi hayo "Nataka tu kuwaambieni kuwa pia katika nchi tajiri kama yetu, kuna migogoro mikubwa kuhusu hili, na tunapaswa kuitatua vyema na kikamilifu na hivyo basi yapo mazungumzo magumu. Tunafahamu kuwa Ujerumani – kama nchi ambayo hutumia kiasi kikubwa cha makaa ya mawe – inapaswa kutoa mchango mkubwa katika kutimiza malengo haya, lakini tutakutana katika siku zijazo na kujadili jinsi ya kulitatua hilo".

Wanaharakati wa mazingira walimtaka Merkel kutangaza mpango wa Ujerumani kuwachana na matumizi ya makaa yam awe katika mazungumzo haya ya Bonn. Ujerumani kwa sasa inapata karibu asilimia 40 ya umeme wake kutoka kwa makaa ya mawe.

UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Merkel asema suala la makaa ya mawe litajadiliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizitaka nchi zote kuharakisha mchakato wa kuhamia katika nishati jadidifu ili kubapambana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia kupunguza athari ambayo inaletwa na hatua ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa. "Kama tutaendelea, tutakubali kimyakimya kuwa ifikapo mwaka wa 2100, orodha ya watu wanaoishi sasa haitaponea. Hatujajiandaa kukubali hilo".

Rais huyo amesema Ufaransa itafidia upungufu wa ufadhili wa utafiti wa kisayansi uliosababishwa na kuondoka kwa Marekani, na itaondoa viwanda vyote vya umeme vinavyoendeshwa na makaa ya mawe ifikapo mwaka wa 2021.

Wiki iliyopita, Syria ilikuwa nchi ya 196 kusaini rasmi makubaliano hayo na kuiacha Marekani kama taifa pekee mwanachama wa Umoja wa Mataifa linaloyapinga.

Makubaliano ya Paris yanazitaka nchi kupunguza kiwango cha wastani cha joto ulimwenguni kuwa chini ya nyuzijoto mbili ili kuepusha athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi kama vile vimbunga, kiangazi na kupanga kwa viwango vya bahari.

Katika kutimiza hilo, mataifa yaliwasilisha ahadi za hiari za kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kutumia nishati inayotokana na nyenzo asili.

UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Emmanuel Macron, Präsident Frankreich
Macron ameahidi ufadhili zaidi katika utafiti wa kisayansiPicha: Getty Images/AFP/L. Schulze

Kwa siku kumi zilizopita, watendaji wa serikali wamekuwa wakijadili kuhusu sheria za kuutekeleza mkataba wa Paris ambazo zitafafanua jinsi nchi lazima zifanye hesabu na kuripoti mchango wao kwa upunguzaji wa gesi chafu duniani.

Kuanzia jana, ilikuwa zamu ya mawaziri wa nishati na mazingira kujadili kuhusu suala la malipo.

Huku akiyataba mabadiliko ya tabianchi kuwa "kitisho kikubwa" Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema uwekezaji unaoendelea kufanywa katika nishati ya kuchafua mazingira inayotokana na nyenzo asilia unahakikisha kuwa hali ya baadaye isiyoweza kuthibitika.

Guterres, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hapo jana waliwasili Bonn kuongoza juhudi za kidiplomasia ili kuyafufua mazungumzo hayo ambayo yamekwama katika suala la fedha.

Ripoti iliyotolewa jana ilionya kuwa kujiondoa kwa Marekani kutoka mkataba wa Paris kutaongeza joto la ulimwengu kwa karibu nusu ya nyuzujoto ifikapo mwka wa 2100, na kufika jumla ya nyuzijoto 3.2.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman