1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Machinjio ya Ujerumani yamulikwa

25 Juni 2020

Kashfa ya maambukizi ya virusi vya Corona katika machinjio ya wanyama inaendelea kugonga vichwa vya habari hususan baada ya miji miwili kurejeshwa chini ya vizuizi kutokana na ongezeko la kasi ya maambukizi mapya.

https://p.dw.com/p/3eJem
Deutschland Arbeiter in Schlachthof
Picha: Getty Images/S. Gallup

Meya wa mojawapo ya miji iliyoathiriwa, amemshutumu mmiliki wa machinjio hayo, kwa mazingira mabovu ya kazi katika kampuni yake. 

Meya huyo, Henning Schulz ambaye mji wake wa Gütersloh hivi sasa umekuwa gumzo Ujerumani baada ya kuzuka kwa mlipuko wa virusi vya Corona amesema wakaazi wa mji huo wana hasira.

Meya huyo amemnyooshea kidole cha lawama mmiliki wa kiwanda cha kichinjio hicho kufuatia mazingira yasioridisha yaliyosababisha kuzuka upya kwa virusi vya Corona.

"Hisia zangu ziko katikati baina ya hasira, huzuni na uchovu. Kwa wakati huu tunajaribu kadri ya uwezo wetu kudhibiti hali inayotukabili" Schulz ameiambia DW.

Meya huyo ameyasema hayo baada ya zaidi ya wafanyikazi 1,500 kukutikana na virusi vya Corona katika kiwanda machinjio  kilichoko mjini Gütersloh na kulazimisha mamlaka katika jimbo la North Rhine-Westphalia kuweka vikwazo vya kutotoka nje mjini humo pamoja na mji jirani wa Warendorf ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Miji hiyo miwili, Gütersloh na Warendorf ina takriban wakaazi 628,000.

Henning Schulz azionya kampuni dhidi ya kutozingatia sheria

Deutschland | Coronavirus | Lockdown Gütersloh | Rheda-Wiedenbrück | Tönnies
Kiwanda cha machinjio cha TönniesPicha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Akizungumza na DW meja Schulz amezionya kampuni zenye kuajiri wafanyakazi dhidi ya kutozingatia sheria, akisisitiza kuwa suala pekee na kampuni zinazohusika na biashara ya nyama.

Mamlaka katika jimbo la North-Rhine Westphalia pia zimezifunga shule, kumbi za michezo, vilabu, pamoja na sehemu zote za mikusanyiko ya umma.

Vile vile, watu wawili tu ndio wanaoruhusiwa kukutana katika sehemu za umma. Mamlaka hiyo imesema kuwa hatua hizo zitadumu angalau kwa wiki moja.

Mnamo siku ya jumatano, waziri mkuu wa jimbo la North-Rhine Westphalia Armin Laschet alieleza kuwa ni janga kubwa kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona katika kiwanda hicho cha kichinjio.

Hata hivyo, maafisa wameonyesha kuridishwa na idadi ndogo ya watu waliopatikana na virusi baada ya zoezi la upimaji wa watu nje ya kiwanda hicho. Katika vipimo vilivyofanyiwa watu 230, wote walipatikana kuwa salama isipokuwa kesi moja tu ambayo matokeo yake hayakubainika mara moja.

Kufuatia mlipuko huo, baadhi ya majimbo hapa Ujerumani tayari yameweka vikwazo kwa wageni wanaotokea katika sehemu zilizoathirika na mlipuko huo kama vile mji wa Gütersloh.

Sasa ni lazima kwa mtu kuwa na cheti cha matibabu kuonyesha kuwa hana virusi vya Corona kabla ya kuruhusiwa kuingia katika majimbo ya Bavaria na Lower Saxony.