1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Vifo nchini Marekani vyakaribia laki moja

Sylvia Mwehozi Mhariri: Rashid Chilumba
24 Mei 2020

Raia wa Marekani wameanza kumiminika katika fukwe za bahari kutokana na hali nzuri ya hewa. Rais Donald Trump naye ajimwaga uwanjani kucheza Gofu lakini chini humo vifo vya COVID -19 vyakaribia 100,000.

https://p.dw.com/p/3cgmr
USA Gouverneur Chris Christie mit Familie am Strand der offiziellen Sommerresidenz
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Mills

Marekani imeorodhesha vifo 1,127 zaidi kutokana na kirusi cha corona na hadi kufikia sasa idadi jumla ya vifo imefikia 97,048 huku kiwango cha maambukizi kimefikia 1,621,658.

Rais Trump ameonekana akicheza Gofu huku wakaazi wa Marekani wakijianika juani wakati hatua za vizuizi zikianza kulegezwa nchini humo. Trump ambaye anataka makanisa, masinagogi na misikiti kuruhusiwa haraka kuendesha ibada, hakuwa amevaa barakoa wakati alipokuwa akicheza Gofu, na hata wachezaji wenzake nao hawakuvaa Barakoa.

Wakati huo huo wamarekani wengi walio na shauku na sikukuu ya mashujaa wikiendi hii wamemiminika kwenye fukwe na maeneo ya nje. Siku hiyo huadhimishwa Jumatatu ya mwisho ya mwezi Mei kila mwaka kuwakumbuka wale waliopoteza maisha wakihudumu katika majeshi ya Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Uhispania

Uhispania itafungua tena milango kwa ajili ya watalii wa nje kuanzia mwezi Julai, baada ya serikali kuahidi kwamba itahakikisha usalama wa wageni na wenyeji. Zaidi ya watalii milioni 80 huwa wanaitembelea Uhispania kwa mwaka. Mnamo mwaka uliopita, Wajerumani milioni 11 walifanya utalii katika nchi hiyo ambayo sasa inahofia kwamba takwimu hizo zitaporomoka.

Waziri mkuu Pedro Sanchez amesema mpango wa euro bilioni 3 wa kuzisaidia familia zilizoathirika zaidi na janga la mripuko wa virusi vya corona, utaanza kufanya kazi katika wiki zinazokuja. "Ninatangaza kwamba kuanzia mwezi Julai, Uhispania itafungua milango kwa ajili ya watalii kwa masharti ya kuzingatia usalama. Watalii wa kigeni wanaweza kuanza kupanga likizo zao katika nchi yetu. Uhispania inahitaji utalii na utalii unahitaji usalama hasa kule unakotoka na unakoenda. Tunaahidi kwamba watalii hawatokuwa hatarini au kuleta kitisho katika nchi", alisema Sanchez.

Waziri huyo mkuu pia ametangaza kurejea kwa ligi kuu ya kandanda nchini Uhispania La Liga kuanzia Juni 8.

Huko Brazil, taifa hilo limetangaza ongezeko la vifo 965 katika taarifa zake za kila siku na kufanya idadi jumla ya vifo kufikia 22,013, kulingana na wizara ya afya. Taifa hilo la Amerika ya Kusini hadi sasa limethibitisha kesi 347,398 za maambukizi ya COVID-19, imesema wizara ya afya, baada ya ongezeko la kesi 16,508 ndani ya kipindi cha saa 24 na kuipita Urusi katika nafasi ya pili duniani ya nchi zilizoathirika zaidi na janga hilo baada ya Marekani.

Shirika la afya duniani WHO, hivi karibuni lilitangaza kwamba bara la Amerika ya Kusini sasa ndio kitovu cha kirusi cha corona.

Makanisa nchini Ufaransa yanajitayarisha hii leo kwa ajili ya ibada ya kwanza katika kipindi cha miezi miwili baada ya serikali kutoa uamuzi kwamba huduma za kidini zinaweza kuendelea chini ya hatua za tahadhari.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi