1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAR ES SALAAM : Wanadiplomasia wajadili Somalia

10 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCTd

Wanadiplomasia wa Ulaya, Afrika Waarabu na Marekani hapo jana wamesisitiza haja ya kuwepo kwa mazungumzo ya pande zote husika juu ya mustakbali wa Somalia ili kuhakikisha utulivu nchini humo pamoja na kuisaidia serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Wakati wa mkutano wa siku moja wa Kundi la Kimataifa la Mawasiliano juu ya suala la Somalia katika mji mkuu wa kibiashara wa D’salaam nchini Tanzania waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe amesema mazungumzo hayo yanapaswa kuwajumuisha wababe wa vita wa Somalia,viongozi wa jimbo lililojitenga la Somaliland na viongozi wa Muungano wa Mahkama za Kiislam waliotimuliwa nchini Somalia.

Wanadiplomasia hao wamemaliza mkutano huo uliofanyika hapo jana bila ya kutowa taarifa lakini Membe amewaambia waandishi wa habari kwamba Tanzania imekubali kuwafunza askari 1,000 wa Somalia katika wiki za hivi karibuni ili kuwaandaa kuchukuwa nafasi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika kinachopangwa kutumwa nchini Somalia siku za mbele.

Wakati mkutano huo ukifanyika mjini D’salaam mamia ya waandamanaji katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu hapo jana wametishia kuwashambulia wanajeshi wa kulinda amani wa Kiafrika na wameziunguza moto bendera za mataifa yanayounga mkono wazo hilo.