1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Denmark na Marekani ziliwapeleleza Merkel, Steinmeier

Lilian Mtono
31 Mei 2021

Taarifa za uchunguzi zilizochapishwa na vyombo vya habari vya nchini Ujerumani zimesema Denmark iliisaidia idara ya usalama wa taifa ya Marekani, NSA kuwapeleleza viongozi wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3uEQW
Deutschland Coronavirus - Impfgipfel
Picha: Annegret Hilse/Reuters/dpa/picture alliance

Taarifa za uchunguzi zilizochapishwa na vyombo vya habari vya nchini Ujerumani zimesema Denmark iliisaidia idara ya usalama wa taifa ya Marekani, NSA kuwapeleleza viongozi wa Ulaya ikiwa ni pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. 

Soma Zaidi: Kerry, Steinmeier wazungumzia ulinzi wa faragha,

Ufichuzi huo ulioonyesha Marekani imekuwa ikiwapeleleza washirika wake kwa mara ya kwanza ulibainishwa mwaka 2013, lakini katika kipindi hiki waandishi wa habari wamefanikiwa kupata taarifa za kina zinazoonyesha msaada ambao Marekani iliupata kutoka kwa shirika la ujasusi la Denmark, FE. 

Ripoti hiyo iliyochapishwa jana Jumapili imeonyesha Denmark ambayo ni mshirika wa karibu wa Ujerumani na jirani yake ilisaidia Marekani kwenye operesheni zake za upelelezi zilizowalenga kansela Angela Merkel na rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Würzburg Mozartfest Eröffnungskonzert | Rede Steinmeier
Rais wa shirikisho la Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ppia amekumbwa na upelelezi huo wa NSA.Picha: Dita Vollmond

Aliyewahi kuwa mgombea wa ukansela wa chama cha mrengo wa wastani wa kushoto SPD, Peer Steinbrück pia alilengwa kwenye upelelezi huo, ripoti hiyo mpya imesema.

Kulingana na ripoti hiyo, duru za kiintelijensia ziliyapelekea kwa siri ripoti hiyo, mashirika ya habari ya Norway, Denmark na Denmark ya DR, STV na NRK pamoja na gazeti la Ufaransa la Le Monde na gazeti la Ujerumani la Süddeustche pamoja na mashirika ya utangazaji ya umma ya NDR na WDR.

Steinbrück alipozungumza na timu ya watafiti ya Ujerumani kuhusiana na ufichuzi huo amesema, kisiasa anautazama kama kashfa huku kansela Merkel na rais Walter Steinmeier wakiwa bado hawajajua chochote kuhusiana na upelelezi huo ulioongozwa na maafisa wa serikali ya Denmark. Msemaji wa Merkel amesema kansela amearifiwa kuhusiana na ufichuzi huo.

Ni kwa namna gani serikali ya Denmark imehusika?

Symbolbild Spionage Affäre
Picha inayoonyesha mfumo wa upelelezi wa kijasusi Picha: Andreas Franke/picture alliance

Serikali ya Denmark ilijua uhusika wa idara yake ya ujasusi kwenye kashfa ya NSA ya Marekani tangu mwaka 2015. Ilianza kukusanya taarifa kuhusiana na ushirikiano kati ya idara hiyo na ile ya Marekani kati ya mwaka 2012 na 2014, katika ripoti ya siri ya Dunhammer kufuatia ufichuzi wa mfanyakazi wa zamani wa NSA na mtoa siri Edward Snowden hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la NDR.

Taarifa walizozikusanya hatimaye zilionyesha wazi kwamba FE iliisaidia NSA kuwapeleleza wanasiasa nchini Sweden, Norway, Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani, lakini pia ilipeleleza wizara za nchi hiyo za mambo ya nje na fedha pamoja na mtengenezaji wa silaha wa Denmark. Walishirikiana pia hata kupeleleza operesheni dhidi ya serikali ya Marekani.

Nini kilichoisukuma FE kuisaidia NSA?

Maalamu mmoja wa operesheni za usalama wa taifa nchini Denmark Thomas Wegener Friis anaamini kwamba FE ilijikuta katika njia panda kuhusiana na mshirika yupi hasa wa kimataifa inaweza kushirikiana naye kwa karibu zaidi. Ameiambia NDR kwamba waliamua wazi kabisa kushirikiana na Marekani dhidi ya washirika wao wa Ulaya.

NSA, FE na wizara ya ulinzi ya Denmark hawakutaka kuzungumzia ripoti hiyo walipotakiwa kufanya hivyo, ingawa taarifa ya jumla kutoka kwa wizara ya ulinzi ilisema kwamba upelelezi wa kimfumo dhidi ya washirika wa karibu haukubaliki.

Mashirika: DW