1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djinnit ahimiza wanawake wapewe nafasi za uongozi Afrika

Reuben Kyama14 Februari 2019

Nchi zinazokabiliwa na misukosuko na mapigano katika ukanda wa Maziwa Makuu zahimizwa kutoa nafasi zaidi kwa wanawake katika nyadhifa za uongozi ili kuwashirikisha katika mchakato wa kuleta amani.

https://p.dw.com/p/3DM8e
Afrika Said Djinnit Sonderbeauftragter UN
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu, Said Djinnit amezitaka nchi za ukanda huo zinazokabiliwa na misukosuko na mapigano ya mara kwa mara kutoa nafasi zaidi kwa wanawake katika nyadhifa za uongozi ili kuwashirikisha katika mchakato wa kuleta amani ya kudumu kwenye eneo hilo. Kauli hiyo ameitoa jijini Nairobi, Kenya alipoongoza mkutano wa kimataifa kuhusu mchango wa wanawake katika suala la kutafuta amani na mapatano katika nchi za ukanda huo. 

Djinnit amesema uchaguzi wa hivi karibuni uliofanyika katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo unaashiria kwamba kuna uwezekano wa kufikia hali ya amani na mapatano katika eneo hilo. Djinnit ameendelea kusema: ''Tunataraji kwamba wakati huu ambapo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeondokana na mchakato wa zoezi la uchaguzi basi tunatazamia kuwa wanawake watapewa nafasi katika nyadhifa za uongozi katika nchi hiyo''.

Amesema wanawake wana ushawishi mkubwa katika kushinikiza amani na mapatano ukizingatia kwamba akina mama na watoto ndio waathiriwa wakuu katika mataifa yanayokabiliwa na majanga au vita na migogoro ya kisiasa.

Rais wa zamani wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza
Rais wa zamani wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-PanzaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Aliyekuwa Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba-Panza pia alikuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo wa siku moja uliohudhuriwa pia na viongozi wanawake wa ngazi za juu kutoka nchi za Maziwa Makuu, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi kutoka mashirika ya kijamii.

Wasemaji katika mkutano huo wamesisitiza umuhimu wa watu kuheshimu haki za binadamu. Wamekemea vikali vitendo vya dhulma dhidi ya wanawake katika nchi kama vile Sudan Kusini ambapo kumekuwa na ongezeko la visa vya ubakaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia kwa ujumla. 

Miongoni mwa nchi zilizowakilishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Pia wajumbe kutoka Umoja wa Afrika na wawakilishi kutoka shirika la maendeleo ya Ujerumani GIZ ni miongoni mwa mataifa mengine ya Ulaya.

Mwandishi: Reuben Kyama

Mhariri: Grace Patricia Kabogo