1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djotodia akabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu

9 Januari 2014

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika ya Kati wanakutana nchini Chad, kuujadili mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na hatima ya rais wa nchi hiyo Michel Djotodia anayeshinikizwa kujiuzulu

https://p.dw.com/p/1Anfr
Zentralafrikanische Republik Vereidigung Michel Djotodia
Picha: STR/AFP/Getty Images

Duru za kisiasa mjini Bangui na duru za kiplomasia za Ufaransa zinasema Djotodia huenda akatangaza kujiuzulu kwake katika mkutano wa kilele wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika ya Kati katika mji mkuu wa Chad, D'Njamena au muda mfupi wakati atakaporejea mjini Bangui.

Msemaji wa Djotodia, ambaye alitwaa madaraka mwezi Machi kama kiongozi wa waasi wa Seleka, amekanusha kuwepo mpango wowote wa aina hiyo. Lakini Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Ahmat Allami amesema viongozi wa kikanda watamuambia Djotodia kuwa serikali yake ya mpito haifanyi kazi.

Allami amesema na namnukuu, “kama hauwezi, kama hauna mamlaka katika hali kama hiyo, basi waondokee wengine wenye uwezo wa kufanya kazi nzuri.” Ahmat hata hivyo amesema kuwa suala la kuubadilisha utawala wa Afrika ya Kati, au serikali ya mpito halitapewa kipau mbele katika mkutano huo. Mada kuu itakayojadiliwa ni hatua za kurejesha amani na usalama nchini humo.

Mjini Bangui, Waziri wa Mawasiliano Guy Simplice Kodegue amesema suala la kumtaka Djotodia ajiuzulu haliko kwenye mada kuu za mkutano wa leo. Ameonya kama suala hilo litajadiliwa, basi nchi hiyo itaendelea kuteketea.

Msafara wa majeshi yanayoendesha zoezi la kuwapokonya silaha waasi mjini Bangui
Msafara wa majeshi yanayoendesha zoezi la kuwapokonya silaha waasi mjini BanguiPicha: P.Pabandji/AFP/GettyImages

Duru za kidiplomasia zimesema maafisa wa Umoja wa Ulaya wamependekeza kwamba Umoja wa Ulaya utume haraka kikosi cha angalau wanajeshi 700 hadi 1,000, katika upande wa magharibi mwa nchi hiyo au mji mkuu Bangui.

Duru kutoka Ufaransa, zimesema Mkutano huo wa N'Djamena utajadili mapendekezo kadhaa ya kuchukuliwa katika kuuendeleza mchakato wa kipindi cha mpito, ikiwa ni pamoja na kumkubalia rais wa Baraza la Taifa la Mpito kuchukua usukani au Waziri Mkuu Nicolas Tiangaye apewe mamlaka ya kuongoza nchi hiyo hadi uchaguzi uandaliwe, ifikapo mwishoni mwaka. Chaguo la tatu huenda likawa ni kuunda timu mpya kabisa ya mpito ijapokuwa hilo huenda likachukua muda mwingi na kuongeza kitisho cha usalama nchini humo.

Kuna hofu kuwa mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati unasambaa katika eneo hilo zima, huku afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa akionya kuwa waasi wa Seleka, na wanajeshi wa zamani wa nchi hiyo wamevuka mpaka na kuingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako wamewafanya watu kukimbia makwao. Djotodia ambaye aliwekwa madarakani kama rais wa mpito chini ya mpango uliosimamiwa na viongozi hao wa kikanda mwaka jana, hajakuwa na uwezo wa kusitisha umwagaji damu ambao pia umesababisha watu milioni moja kubaki bila makaazi na kuzusha hofu ya kutokea tena mauwaji ya halaiki kama yaliyotokea Rwanda mwaka wa1994.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Ssessanga, Iddi