1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Donald Trump adaiwa kudanganya benki ili kupata mikopo

Lilian Mtono
27 Septemba 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anashitakiwa na mwanasheria mkuu wa New York kwa kudanganya benki na bima kwa kuongeza thamani ya mali zake. Uamuzi wa jaji unapunguza uzito wa kesi nyingine dhidi yake wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4WqKO
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba kwenye kongamano la wanawake katika sekta ya sheria, (CWALAC) Septemba 15, 2023
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba kwenye kongamano la wanawake katika sekta ya sheria, (CWALAC) Septemba 15, 2023 Picha: Leah Millis/REUTERS

Mahakama ya New York imetoa uamuzi jana Jumanne kwamba aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trumpalifanya ulaghai katika shughuli zake za biashara katika muongo mmoja uliopita. Madai haya ni sehemu ya kesi ya madai dhidi ya Trump.

Jaji Arthur Engoron, alipokuwa akitoa uamuzi wa kesi hiyo iliyowasilishwa na mwanasheria mkuu wa serikali wa New York Letitia James, amesema Trump na kampuni yake waliidanganya benki, makampuni ya bima na wengineo kwa kutoa tathmini ya uongo ya mali zake ili kupata mikataba na mikopo.

Jaji Engoron aidha ameamuru kufutwa baadhi ya leseni za biashara za Trump kama adhabu na kumuwekea mazingira magumu ya kufanya biashara mjini New York na kuongeza kuwa ataweka mfuatiliaji huru atakayeendelea kusimamia operesheni za mtandao wa kibiashara wa Trump.

Soma pia:Trump kuomba kubadilishiwa jaji 

Wakili wa Trump, Christopher Kise amesema wanaweza kuukatia rufaa uamuzi huo aliouita "upotoshaji wa haki" na usiozingatia hata kidogo ukweli na sheria.

Pamoja na kesi zinazomkabili, Trump bado ana uungwaji mkono katika nia yake ya kuwania tena urais katika uchaguzi wa mwakani
Pamoja na kesi zinazomkabili, Trump bado ana uungwaji mkono katika nia yake ya kuwania tena urais katika uchaguzi wa mwakaniPicha: Marco Bello/REUTERS

Kwa muda mrefu, Trump amekuwa akisisitiza hajafanya kosa lolote. Mtoto wake wa kiume Eric, amesema uamuzi huo wa Engoron "ni jaribio la kumpoteza baba yake na kumfukuza New York." Eric na mtoto mwingine wa Trump, Don Jr, pia wanahusishwa na madai hayo.

Eric ambaye ni mtendaji mkuu wa biashara za Trump ameandika kwenye mtandao wa X, "Leo, nimepoteza imani na mfumo wa kisheria wa New York."

Soma pia: Trump asema hataacha kuwania urais

Ameongeza "Sijawahi kuona chuki kama hii ya jaji dhidi ya mtu mmoja- juhudi za kupangwa pamoja na mwanasheria mkuu kuharibu maisha ya mtu, kampuni na mafanikio yake."

Madai ya New York yanasemaje?

Mwanasheria mkuu wa New York amedai kwamba Trump aliongeza thamani ya mali yake kwa kiasi cha dola bilioni 2.23, kwenye taarifa za fedha za kila mwaka alizoziwasilisha benki na kampuni ya bima.

Jumba la kifahari la Donald Trump lililoko Mar-a-Lago, Florida ambalo ni moja ya mali alizoziongezea thamani ili kudanganya benki na bima
Jumba la kifahari la Donald Trump lililoko Mar-a-Lago, Florida ambalo ni moja ya mali alizoziongezea thamani ili kudanganya benki na bimaPicha: Steve Helber/AP Photo/picture alliance

James alidai kuwa Trump alifanya hivyo "ili kuendelea kupata mikopo na bima kwa masharti nafuu zaidi."

Soma pia: Trump kufika tena mahakamani

Mali alizoziongezea thamani ni pamoja na jumba lake la kifahari la Mar-a-Lago, Florida, majengo ya ofisi na viwanja vya mchezo wa gofu pamoja na nyumba yake iliyoko ghorofa ya juu katika jengo la Trump Tower, ambayo aliiongeza mara tatu ya ukubwa wake halisi.

Nini kitarajiwe?

Uamuzi wa Engoron unapunguza masuala ambayo pengine yangesikilizwa katika kesi nyingine ya wiki ijayo. Imeweka wazi kwa ufasaha kabisa kiini cha kesi ya James kuwa halali, gazeti la New York Times liliripoti.

Kesi hii iliwasilishwa na Letitia na ofisi ya mwanasheria mkuu ya jimbo Septemba 2022.

Trump anakabiliwa na mashtaka mengine ya uhalifu ambayo ni pamoja na jukumu lake katika ghasia za jengo la bunge "Capitol Hill", kuingilia uchaguzi katika jimbo la Georgia, ukiukaji wa kanuni za kutunza nyaraka za siri, pamoja na kashfa ya kumlipa pesa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels ili asifichue mahusiano waliyokuwa nayo.

Soma pia: Je, Trump anataondolewa kuwania urais mnamo Januari 6?