1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump ziarani Bethlehem

Oumilkheir Hamidou
23 Mei 2017

Rais Trump wa Marekani anaendelea na ziara yake Mashariki ya kati. Amekutana na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina Mahmoud Abbas na ataweka shada la mauwa katika kumbusho la Yad Vashem kabla ya kuelekea Vatikan.

https://p.dw.com/p/2dQb9
USA Donald Trump PK mit Mahmoud Abbas in Bethlehem
Picha: Reuters/M. Torokman

 

Rais huyo wa Marekani amekaribishwa na Mahamoud Abbas katika kasri la rais mjini Bethlehem , baada ya mlolongo wa magari yaliyofuatana nae kupita katika njia unakokutikana ukuta uliojengwa na Israel pamoja pia na kivukio mashuhuhuri, kinachoamuru kufunguliwa njia ya kuingia Bethlehem. Kwa namna hiyo rais Trump amejionea mwenyewe ukweli wa hali ya mambo namna ulivyo katika mzozo mmojawapo mkongwe kabisa wa dunia.

Katika mazungumzo pamoja na waandishi habari mwishoni mwa mazungumzo yake pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina mjini  Bethlehem, rais Trump ameahidi "kufanya kila liwezekanalo" kuwasaidia waisrael na wapalastina kufikia makubaliano ya amani.

Rais Trump (kushoto) akizungumza na waziri mkuu wa Israel Netanyahu
Rais Trump (kushoto) akizungumza na waziri mkuu wa Israel NetanyahuPicha: Reuters/Courtesy of Government Press Office/Kobi Gideon

Wapalastina na  Waisrael wako tayari kushirikiana na Trump kusaka amani

"Amani ndio chaguo tunalobidi kuwa nalo kila siku na Marekani tuko tayari kusaidia kuifikia ndoto hiyo" amesema rais Trump mbele ya kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas, aliyekutana nae ana kwa ana hapo awali. Ameongeza kusema, Mahmoud Abbas amemhakikishia utayarifu wake wa kushirikiana kwa dhati ili kulifikia lengo hilo na kwamba waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia amemhakikishia hayo hayo alipokutana nae jana.

Rais Trump amesema "makubaliano ya amani pamoja na Israel yatafungua njia ya kupatikana amani katika eneo lote la mashariki ya kati."Rais wa Marekani ametilia mkazo umuhimu wa kuufufua uchumi wa wapalestina anaosema uko katika hali mbaya kupita kiasi.

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis
Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa FrancisPicha: picture-alliance/NurPhoto/P. Fiuza

 Trump ataelekea Vatikan baadae leo kwa mazungumzo na Papa Francis

Baadae hii leo rais Trump atarejea Jerusalem atakakolizuru kumbusho la wahanga wa mauwaji ya halaiki yaliyofanywa na wanazi katika vita vikuu vya pili vya dunia Holocaust- Yad Vashem na kuhutubia. Baadaye rais Trump anapanga kuelekea Roma, ambako atakutana na kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis huko Vatikan.

Ziara ya rais wa Marekani mjini Bethlehem imegubikwa na shambulio la kigaidi la mjini Manchester ambalo viongozi wote wawili, Donald Trump na Mahmoud Abbas wamelilaani vikali.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/PA/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman