1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yataka kikosi cha MONUSCO kuondoka

Sylvia Mwehozi
4 Aprili 2018

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inataka ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo ifikapo mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/2vU4a
Semuliki, Nord-Kivu, DR Kongo: Der Untergeneralsekretär der Vereinten Nationen für Friedenssicherungseinsätze, Jean-Pierre Lacroix, besuchte heute den Stützpunkt Semuliki
Picha: Monusco/A.Khan

Uamuzi huo unakuja kufuatia baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kupiga kura wiki iliyopita ya kurefusha  mamlaka ya walinzi wa amani kwa mwaka mwingine. 

Waziri wa mambo ya nje wa Congo Leonard She Okitundu amesema wameliarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba mamlaka ya sasa yanachukuliwa kuwa ya mwisho, kabla ya vikosi hivyo kuondoka moja kwa moja katika taifa hilo baada ya kuwepo miaka 20.

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya mgogoro wa kibinadamu unaongezeka huko DRC, ambapo watu angalau milioni 13 wanahitaji misaada ya kiutu, wakiwemo milioni 7.7 ambao hawana uhakika wa chakula. Baraza la Usalama siku ya jumanne liliupatia wajibu mkubwa ujumbe wa kulinda amani nchini DRC, kusaidia kuandaa uchaguzi utakaomaliza utawala wa rais Joseph Kabila.

Baraza hilo lilipitisha azimio lililowasilishwa na Ufaransa linalotoa mamlaka mapya ya kikosi cha MONUSCO hadi Machi 2019 na kusisitiza umuhimu wa kuwalinda raia wakati DRC ikielekea katika uchaguzi wa kihistoria Desemba mwaka huu.

Joseph Kabila Präsident der Demokratischen Republik Kongo
Rais Joseph Kabila anayekabiliwa na shinikizo la kukabidhi madaraka kwa amaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Urusi ilionya kwamba ujumbe wa kulinda amani hautakiwi kuwa na upande wowote katika uchaguzi wa nchi hiyo wakati balozi wa Kongo akisema kwamba lengo la kikosi hicho iwe ni kupambana na makundi ya waasi na sio kuunga mkono uchaguzi.

She Okitundu ambaye ni waziri wa mambo ya nje na naibu waziri mkuu, siku ya Jumanne alikumbusha kuwa Kabila aliueleza Umoja wa Mataifa Septemba iliyopita kwamba "vikosi vya Umoja huo haviwezi kushikwa na tamaa ya kukaa milele". She Okitundu alithibitisha kwamba Kongo haitahudhuria mkutano wa wafadhili mjini Geneva Aprili 13 unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya, kwa ajili ya kukusanya kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 1.7 ili kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu wa Kinshasa.

Mwezi uliopita waziri mkuu Jose Makila alisema kwamba Umoja wa Mataifa unatoa tuhuma zilizopitiliza na kwamba mashirika ya kimsaada katika nchi hiyo yanafanya propaganda ya kueneza picha mbaya ya DRC kwa ulimwengu. Kikosi cha MONUSCO ndicho kikosi kikubwa cha Umoja wa Mataifa chenye askari 16,215 na karibu polisi 1450 pamoja na raia.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman