1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DUBAI : Wanamgambo watishia kuuwa mateka wa Ujerumani

10 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKX

Kundi la wanamgambo wa Kiislam lisilojulikana sana nchini Iraq limesema leo hii litawauwa mateka wawili mwanamke wa Kijerumani na mwanawe wa kiume katika kipindi cha siku 10 iwapo serikali ya Ujerumani haitowaondowa wanajeshi wake kutoka Afghanistan.

Kundi hilo linalojiita Mishale ya Haki limeweka ukanda wa video kwenye mtandao wenye kumuonyesha Hannelore Marianne Krause akiisihi Ujerumani kuitikia madai ya wanamgambo hao.

Ukanda huo umewekwa kwenye tovuti leo hii ambayo hutumiwa na makundi ya wanamgambo likiwemo kundi la Al Qaida.

Mtu aliejifunika uso akisoma taarifa kwenye ukanda huo wa video amesema wanaipa serikali ya Ujerumani siku 10 kuanzia siku ya kutolewa kwa taarifa hiyo kutangaza kuanza kuundolewa kwa vikosi vyake kutoka Afghanistan venginevyo hawataweza hata kuziona maiti za kile walichodai majasusi mawili.

Krause mwenye umri wa miaka 61 akiwa amekaa pembeni mwa kijana wa kiume amemsihi Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kutimiza madai ya wateka nyara wake ili kuyaokowa maisha yake na mwanawe wa kiume.Mateka wote wawili walikuwa wakilia wakati mama huyo akitowa ombi lake hilo.

Ujerumani ilipinga uvamizi uliongozwa na Marekani nchini Iraq hapo mwaka 2003.