1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari

Mohammed Khelef
3 Mei 2023

Umoja wa Mataifa na Shirika la Waandishi wa Habari Bila Mipaka wanasema mashambulizi dhidi ya uhuru wa habari yako kila kona ya ulimwengu, ambapo waandishi wameendelea kuteswa, kufungwa na hata kuuawa.

https://p.dw.com/p/4Qplr
BdTD Protest der Palästinenser gegen die israelische Blockade von Gaza
Picha: Reuters/M. Salem

Akitumia ujumbe wa video kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema siku ya Jumatano (Mei 3) kwamba kila uhuru duniani "unategemea moja kwa moja uhuru wa habari, akiuita uhuru huo kuwa ndio msingi wa demokrasia na haki na damu kwenye uhai wa haki za binaadamu."

Hali ya uhuru wa vyombo vya habari ikoje nchini mwako?

Hata hivyo, katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema ni jambo la kusikitisha kwamba kila kona ya ulimwengu leo hii inashuhudia mashambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari yakiongezeka.

Soma zaidi: 

RSF: Mazingira ya kifo cha mwandishi wa habari Rwanda hayakuwa wazi

"Ukweli unatishiwa na habari za uongo na kauli za chuki, ambazo zinajaribu kuweka ukungu baina ya ukweli na uzushi, baina ya sayansi na dhana potofu. Na waandishi wa habari wanaendelea kubughudhiwa, kutishwa, kuwekwa vizuizini na magerezani." Aliongeza Guterres.

Wanahabari 59 wauawa


 Kwa mujibu wa Shirika la Waandishi wa Habari Bila Mipaka, jumla ya wanahabari 59 waliuawa wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi katika mwaka uliopita wa 2022.

Frankreich I Nach Tod von Journalistin im Westjordanland - Proteste
Mmoja wa waandamanaji akiwa amebeba picha ya mwandishi wa habari wa Kipalestina aliyeuawa na majeshi ya Israel mwezi Septemba 2022, Shireen Abu Aqleh.Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance Ilia Yefimovich/dpa

Mkurugenzi wa shirika hilo, Christophe Deloire, amesema miongoni mwa waliouawa ni mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, Shireen Abu Akleh, aliyekuwa akiripoti katika ardhi za Mamlaka ya Palestina, akidai kuwa rikodi ya Israel kwenye suala hili si nzuri. 

Soma zaidi: Mkanganyiko kuhusu muswada wa huduma za habari Tanzania

"Hakuna anayepaswa kuzuzuliwa na kinachotokea nchini Israel. Nchi hiyo ni ya 97 katika Faharasa ya Uhuru wa Habari kati ya nchi 180, jambo ambalo ni baya kwa demokrasia. Kuna mambo mengine kadhaa hapana shaka, kuhusu tabia ya vikosi vya Israel ndani ya Palestina, ambapo kukitokea mauaji, hakuna nia, na hata kuna ukaidi, wa Israel kuchunguza kujuwa ukweli. Hiki ndicho kilichojiri pale mwandishi wa habari wa al-Jazeera, Shireen Abu Akleh, alipouawa mwaka mmoja uliopita." Alisema mkurugenzi huyo.

UNESCO yawapa tuzo Wairani watatu

Katika kuadhimisha siku hii, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitowa tuzo yake ya mwaka 2023 ya Uhuru wa Habari Duniani kwa wanawake watatu wa Iran, wawili kati yao wakiwa waandishi wa habari na mmoja mwanaharakati wa haki za binaadamu ambaye yuko jela.

Narges Mohammadi, Niloufar Hamedi und Elaheh Mohammadi
Kutoka kulia, Narges Mohammadi, Niloufar Hamedi na Elaheh Mohammadi, wanawake wa Iran waliotunukiwa tuzo ya UNESCO juu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mwaka 2023.Picha: Shargh

Waandishi wa habari ni Elaheh Mohammadi na Niloufar Hamedi, ambao ndio waliosaidia kufichua kifo cha msichana Mahsa Amini aliyefia akiwa mikononi mwa polisi ya maadili mwezi Septemba mwaka jana na mwanaharakati wa haki za binaadamu ni Narges Mohammadi.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay, alisema zama za dijitali "zinaibadilisha taswira nzima ya upashanaji habari ulimwenguni, na kuifanya tasnia hii kuwa ya kitaalamu zaidi, huru zaidi, na muhimu zaidi" kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla.

Vyanzo: Reuters, AFP